Hunijui kuwa niko mwilini mwako. nakutafuna pole pole. Na mwisho nitakuangusha !
Ugonjwa wa kisukari ni ugonjwa wa mwili kushindwa kuthibiti na kurekebisha kiasi cha sukari mwilini.
Leo
tutaanza makala ya kwanza kati ya makala zaidi ya 30 ya kuelezea juu ya
ugonjwa wa kisukari. Tutaanza kwa kuelezea kisukari ni ugonjwa gani na
kwa kuwa unahusu homoni ya insulini inayotengenezwa na glandi ya
pankrasi tutaanzia kwa kuelezea maana ya systima za mwili, homoni ya
insulini na glandi ya pankrasi. Baadaye tutazungumzia kisukari ni nini,
dalili zake, matatizo yake na matibabu yake. Tutazungumzia vile vile
matatizo ya mama mjamzito wakati ana kisukari.
Tuanze
makala ya kwanza kwa kusema kuwa wanafunzi wanaojifunza kuwa madaktari
huanza kwa kujifunza masomo manne makubwa: anatomia (Anatomy),
fisiologia (physiology), bayokemia ( biochemistry) na pathologia
(pathology). La kwanza, anatomia ni somo la kufahamu muundo wa kila sehemu ya mwili wa mtu, la pili (bayokemia) na la tatu (fisiologia) ni kujua jinsi mwili unavyofanya kazi. Hujifunza, kwa mfano, namna
mwili unavyomeng’enya na kuchanganya vyakula na hewa ili kuzalisha
nishati ya kuendesha mwili. Katika somo la patholojia wanajifunza
mabadiliko yanayotokea kwenye sehemu za mwili wakati zinapoingiliwa na
magonjwa.
Masomo haya manne
ndiyo misingi ya kujifunza na kuelewa juu ya ugonjwa wowote pamoja na
ugonjwa wa kisukari. Kwa mfano, ukitaka kuelezea juu ya ugonjwa wa
kisukari huna budi kuongelea juu ya anatomia na patholojia ya kiungo
kinachotengeneza homoni inayohusika kwenye ugonjwa wa kisukari. Ukitaka
kuelezea kisukari kinavyodhuru jicho huna budi kuongea juu ya anatomia
ya jicho.
Ili kuuelewa ugonjwa wa kisukari, hatuna budi kuyapitia masomo haya manne kwa angalau kiasi kidogo kila inapobidi......
Makundi ya magonjwa
Magonjwa
yanaweza yakagawanyika kwenye makundi mawili muhimu: yanayoambukizwa na
yasiyoambukizwa. Magonjwa yanayoambukizwa ni kama malaria, VVU,
kisonono, safura, TB, kichocho, kichomi, kifua kikuu nakadhalika. Kundi
la pili, yaani magonjwa yasiyoambukizwa lina magonjwa kama ugonjwa wa
presha, kisukari, saratani na magonjwa ya moyo.
Ugonjwa wa kisukari ndio
ugonjwa wenye wagonjwa wengi zaidi katika kundi hili la magonjwa
yasiyoambukizwa. Kuna watu karibu milioni mia moja wenye kisukari
ulimwenguni. Kwa hiyo kama wewe una ugonjwa wa kisukari fahamu tu kwamba
haupo peke yako kwani kuna wenzako milioni mia moja wenye ugonjwa kama
wa kwako.
Systima za mwili
Mwili
umejengwa na vitofali vidogo vidogo vinavyoitwa seli. Mkusanyiko wa
seli za aina mbali mbali zinazoshirikiana katika kufanya shughuli moja
au shughuli mbali mbali unaitwa tishu na tishu mbali mbali zikikusanyika
na kushirikiana kufanya kazi moja au zaidi; mkusanyiko huu unaitwa
kiungo. Mwili una viungo vingi kama ini, figo, ubongo, pankrasi
nakadhalika. Kiungo kinachohusika kwenye ugonjwa wa kisukari kinaitwa pankrasi. Kwenye kiungo hiki kuna seli na tishu mbali mbali. Selli zinazohusika na ugonjwa wa kisukari ni zile zinazotengeneza homoni ya insulini.
Viungo
mwilini vinaungana na kuwa na systima ambayo ni mkusanyiko wa viungo
vikiungana na kufanya shughuli moja au zaidi. Mwilini kuna systima 13 ambazo ni: systima
ya ubongo na neva; moyo, damu na mishipa ya damu; kupumua; kumeng’enya
chakula; kinga; musuli; mifupa; kutoa taka; homoni; ngozi, uzazi na sensi
Glandi ni nini?
Kuna
viungo mbali mbali mwilini moja ikiwa ni kundi ambalo linaitwa ‘glands.’
Hii ni mojawapo ya sehemu ya mwili wetu ambayo bado sijaweza kupata
neno lake la Kiswahili. Kwa sasa tutafsiri neno la kitaalamu ‘glands’
kama glandi kwa Kiswahili. La maana ni kujua kuwa tunazungumzia nini
tukisema mwilini kuna glandi. Mfano wa glandi ni kama zile zinazotoa
machozi na zinazotoa mate. Tezi vile vile ni aina ya glandi. Kazi za
glandi ni kutengeneza vimeng’enyo na homoni. Ziwa ni glandi maana
hutengeneza maziwa na kuyaingiza kwenye mrija na kumpelekea mtoto
anyonye kwenye chuchu ya ziwa.
Kuna
aina mbili za glandi. Moja ni zile ambazo zikishatengeneza vimeng’enyo
huviweka au huvifikisha kwenye mrija ambao utavipeleka huko
vinakohitajika. Ya pili ni pale glandi haina mrija. Kimmeng’enyo au
homoni inayotengenezwa humo huingia moja kwa moja kwenye damu. Glandi
muhimu inayohusika kwenye ugonjwa wa kisukari ni pankrasi. Glandi hii
inatengeneza homoni inayoitwa insulini.
Homoni ni nini?
Systima
ya homoni ni mojawapo ya systima za mwili. Systima hii ni mkusanyiko wa
glandi; kila moja ikitengeneza homoni muhimu za kuendesha, kurekebisha
au kuthibiti shughuli maalumu kwenye mwili. Homoni ni kemikali
zinazotengenezwa na viungo vya systima ya homoni. Homoni
zikishatengenezwa huingia moja kwa moja kwenye damu na kupelekwa kwenye
viungo lengwa zinapohitajika kuendesha, kuthibiti au kurekebisha
shughuli kwenye viungo lengwa.
Mwilini
kuna zaidi ya homoni 50. Kwa hiyo magonjwa yanayotokana na systima ya
homoni ni mengi. Moja ya magonjwa kwenye systima ya homoni ni ugonjwa wa
kisukari. Homoni inayohusika kwenye ugonjwa wa kisukari ni homoni inayoitwa insulini ambayo inatengenezwa na kiungo kinachoitwa pankrasi.
Turudie
kwa kutia msisitizo kuwa moja ya systima kumi na tatu za mwili ni
systima ya homoni. Humo kwenye systima ya homoni kuna glandi ambazo ni
viungo vinavyotengeneza homoni. Homoni ni kemikali zinazotengenezwa na
glandi na kuingia moja kwa moja kwenye damu na kupelekwa
kwenye viungo lengwa zinapohitajika kuendesha, kuthibiti au kurekebisha
shughuli kwenye viungo hivyo. Homoni inayohusika na ugonjwa wa kisukari
inaitwa insulini na inatengenezwa na glandi inayoitwa pankrasi.
Wiki ijayo tutaelezea juu ya kiungo hiki cha pankrasi na kuelezea kinafanya kazi gani,
Wasomaji
tunaomba maswali na maoni yenu kuhusu ugonjwa wa kisukari. Wataalamu
tunaomba mawazo na maoni yenu kupitia e-mail; afyatele@gmail.com
au kupitia kiboksi cha kuandika na kutuma moni, kilichopo pembeni kulia (NB: utakavyovituma vitakuwa ni siri, havitotolewa popote)
0 comments:
Post a Comment