-

-

-

-

-

Habari Mpya

Thursday 4 December 2014

Unayajua Mambo yanayoathiri afya zetu

Mambo yanayoathiri afya zetu
Mazingira ni jambo lingine linaloathiri afya. Iwapo maji tunayokunjwa na kutumia ni safi na salama, iwapo hewa tunayovuta si chafu, maeneo tunayofanyia kazi ni salama na pia nyumba tunazoishi, basi afya zetu huwa salama zaidi ikilinganishwa na watu wanaoishi kwenye maeneo yasiyo na maji safi na salama au kuvuta hewa chafu na kufanya kazi kwenye mazingira ya hatari. Uchunguzi uliofanywa na chuo kikuu cha Zuyd nchini Uholanzi umeonesha kwamba, kuvuta hewa iliyochafuliwa kwa gesi za magari kwa lisaa limoja kunatosha kumpatia mtu mfadhaiko wa kifikra au stress katika ubongo wake. Utafiti mwingine uliofanywa na chuo kikuu cha India cha Purdue umebainisha kuwa, sumu kali inayotokana na sumu ya risasi, inayoweza kuiingia mwilini mwa binadamu kutokana na kula vitu vilivyoingiwa na sumu hiyo, nchini Marekani huathiri maelfu ya watoto kuliko kiwango dhaifu cha sumu hiyo kinachoweza kuwepo katika vifaa vya kuchezea na mapambo yanavyosafirishwa.
Afya ya binadamu pia huweza kuathiriwa na watu wanaomzunguka. Iwapo una familia unayoiangalia au marafiki katika jamii yako, basi una nafasi kubwa ya kuimarisha afya yako kuliko mtu ambaye anaishi pekee au hana familia na marafiki. Uchunguzi uliofanywa na chuo kikuu cha Washington nchini Marekani umegundua kuwa, ushirikiano wa kifamilia ni jambo zuri kwa mtu na hupunguza kesi za atu kujiua, hasa wale wanaopatwa na matatizo ya mfadhaiko wa kifikra au wanapokuwa na fikra ya kutaka kujiua.  Vilevile tamaduni, mila na desturi za jamii na jinsi watu wanavyozithamini itikadi hizo, zina mafasi kubwa katika afya zao ingawa matokeo yake huweza kuwa mazuri au mabaya. Kwa mfano mazoea na mila ya kuwakeketa au kuwatahiri watoto wa kike na wanawake ina madhara makubwa kama vile kuongeza kiwango cha maambukizo ya magonjwa na hata matatizo ya kiakili miongoni mwa wasichama na wanawake wanaofanyiwa jambo hilo. Utafiti uliochapishwa katika Jarida la Afya ya Jamii na  Elimu ya Magonjwa ya Mlipuko umebainisha kuwa, wakati vijana wanapovaa mavazi kwa mujibu wa mila na tamaduni za makundi au makabila yao, suala hilo huweza kuwapunguzia uwezekano wa kupatwa na matatizo ya kiakili baadaye maishani.

Urithi wa jenetiki ni suala jingine linaloathiri afya za watu. Kuishi muda mrefu, siha ya mwili kwa ujumla na kupatwa na baadhi ya magonjwa na hata kuzaliwa nayo, ni masuala yanayoainishwa na jinsi jeni zetu zilivyo mwilini tangu wakati tunapozaliwa. Mambo mengine ni pamoja na vyakula tunavyokula, harakati zetu kifizikia, tabia na mazoea tofauti kama kuvuta sigara au kunywa pombe na kutumia madawa ya kulevya. Pia jinsi tunavyoweza kuvumilia mfadhaiko wa kifikra au stress yote hayo yana nafasi muhimu katika uzima wetu kimwili na kiakili. Suala jingine tunaloweza kulitaja hapa ni matumizi ya vituo vya afya na hospitali. Jamii ambayo ina vituo vya afya vya kutosha, vilivyo vizuri na vyenye kukidhi mahitaji ya watu wa jamii hiyo, watu wake wana nafasi zaidi ya kuwa na siha nzuri kuliko jamii au watu wanaoishi maeneo ambayo hayana vituo vya afya au hospitali. Kwa mfano nchi zilizoendelea zenye vituo vya afya na hospitali za kutosha na nzuri, watu wa nchi hizo huishi maisha marefu zaidi ikilinganishwa na nchi masikini zenye upungufu katika sekta hiyo.  Jinsia ya mtu pia huathiri afya yake. Kuna magonjwa yanayowapata wanawake zaidi na kuna magonjwa yanayowapata wanaume zaidi. Hali ya miili ya wanawake hutofautiana na wanaume na hata kazi na shughuli wanazozifanya pia huweza kuathiri afya zao kwa ujumla. Kwa mfano, kubeba mimba na kujifungua, kansa ya ovari na kizazi huathiri afya ya wanawake katika hali ambayo wanaume hupatwa na kansa ya tezi kibofu na ya korodani. Wakati wa vita wanaume hushiriki kwa wingi kuliko wanawake na matokeo yake ni kuuawa au kujeruhiwa. Wanawake na wasichana huenda wakawa wahanga wa vitendo vya utumiaji mabavu dhidi yao na ukatili kuliko watoto wa kiume na wanaume. Katika baadhi ya jamii watoto wa kike na wanawake huwa hawapewi fursa ya kupata elimu na kujiendeleza kama wanaume, suala ambalo huathiri afya zao pia. Tafiti nyingi zimeonyesha ubaguzi wa kijinsia katika utoaji huduma za afya hata katika nchi zilizoendelea.

Miongoni mwa mambo muhimu yanayoijenga afya ya mwanadamu ni kula lishe salama na mlo uliokamilika. Tunaposema lishe salama na mlo uliokamilika au healthy balanced diet kwa kimombo, tunamaanisha masuala muhimu mawili. Moja ni kula kiwango kinachotakiwa cha chakula kwa mujibu wa harakati na hitajio la mwili wako, na pili ni kula aina tofauti za vyakula vinavyotakiwa ili kuijenga siha ya mwili. Tunapaswa kufahamu kwamba, kula lishe bora ni suala muhimu linalochangia kuimarisha afya ya mwili. Lishe salama na iliyokami inamaanisha kula vyakula tofauti kutoka katika mafungu manne makuu ya vyakula na kupunguza baadhi ya vyakula katika milo tunayokula kila siku.
Aina ya vyakula vinavyopaswa kuwepo kwenye milo yetu ni pamoja na matunda na mboga kwa wingi.  Kiwango cha kutosha cha wanga kama vile mkate, wali, viazi, pasta na vinginevyo na ni bora viwe vinatokana na aina mbalimbali za nafaka kamili zisiokobolewa. Maziwa na vyakula vinavyotokana na maziwa kama mtindi na jibini. Vyakula vyenye protini kama vyama, samaki, mayai, maharagwe na vinginevyo na vilevile kiasi kidogo cha sukari , mafuta na chumvi.

ufuatao ni ushauri au vidokezo muhimu (tips) kuhusiana na namna ya kula vyema ili kuzilinda na kuziimarisha afya zetu.  Tunashauriwa mlo tunaokula uwe na kiasi cha kutosha cha wanga, kwani aina hiyo ya chakula huipa miili yetu nguvu. Tunashauriwa kula matunda na mboga kwa wingi kila siku. Baadhi wanasema, ni bora kula aina 5 za matunda tofauti na mboga kwa siku. Pia tunashauriwa kula samaki kwa wingi kwa uchache mara mbili kila wiki na kama hatutoweza kufanya hivyo au kwa wale ambao samaki wanawadhuru na wale wasiokula nyama, wanapaswa kula virutubishi muhimu vinavyotupatia mada zinazopatikana kwenye samaki kwa ajili ya afya ya miili yetu. Tunashauriwa kupunguza kwa kiasi kikubwa sukari na mafuta katika milo yetu. Vilevile tunashauriwa kula chumvi kwa kiwango kidogo, isizidi gramu 6 kwa siku kwa watu wazima. Tunapaswa kufahamu kuwa, baadhi ya vyakula tayari vina kiwango cha chumvi ndani yake kwani karibu theluthi moja ya chumvi katika milo yetu hutoka katika vyakula ambavyo tayari vimeshatengeneza kama supu iliyo tayari, sosi, mikate, asusa (snacks), pai, pizza vyakula vinavyosindikwa na kuhifadhiwa. Hivyo kuna umuhimu wa kula vyakula hivyo kwa kiasi kidogo. Hii ni kwa sababu ongezeko la chumvi mwilini huweza kumfanya mtu apatwe na shinikizo la damu, hali ambayo huweza kusababisha ugonjwa wa moyo na kiharusi. Suala jingine tunalopaswa kuzingatia ni kunywa maji ya kutosha, tunashauriwa kila siku kunywa kiasi cha gilasi 6 hadi 8 za maji au vyakula vingine vya majimaji kama juisi na kadhalika, ili kuzuia upungufu wa maji mwilini. Maji yana faida nyingi na baadhi yake ni kuusaidia mwili kuondoa kwa urahisi sumu na mabaki yasiyotakiwa mwilini. Kusaidia kulainisha macho na maungio ya mwili na pia hutusaidia wakati wa kumeza.
Jambo jingine tunaloshauriwa ni kuupa mwili harakati, mazoezi ya mara kwa mara na kuwa na uzito unaotakiwa kiafya. Jengine ni kutoacha kula kifuangua kinywa. Tunatakiwa kustaftahi kila siku kwa sababu chakula hicho cha asubuhi huupa mwili nguvu ya kuanzia siku na huamsha utendaji kazi wa mwili kwa ajili ya siku nzima.

 Natumaini mmefaidika na kwa kuwa kuvunjika kwa koleo sio mwisho wa uhunzi basi  panapo majaaliwa.
kwa hisani ya Iran Swahili Radio
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

0 comments:

Post a Comment

Item Reviewed: Unayajua Mambo yanayoathiri afya zetu Description: Rating: 5 Reviewed By: Unknown
Scroll to Top