Tunauongelea ugonjwa wa presha kwa sababu zifuatazo:
- Ugonjwa wa presha ni ugonjwa unaowaathiri watu wengi, unaowaletea watu wengi matatizo ya kiafya, unajificha mpaka yanapoanza matatizo makubwa, ni mojawapo ya viashiria vya hatari kinachoungana na viashiria vingine kusababisha mshtuko wa moyo na kiharusi,
- presha inaviharibu viungo vya mwili kama vile mishipa ya damu, moyo, figo, ubongo na macho;
- ni ugonjwa ambao mtu anaweza akauzuia kwa kiasi kikubwa na kama ukishatokea matibabu yake na maendeleo yake hutegemea sana jinsi mgonjwa anavyofanya bidii kuishi staili ya maisha inayohusiana na kushuka na kuthibiti presha yake.
- Tutaelezea maana ya presha kwenye damu, namna ya kupima presha ya damu, maana ya ugonjwa wa presha, ni nini kinachousababisha, dalili zake, matatizo yake na unavyohusiana na staili za maisha. Makala ya leo tutaelezea maana ya presha yaani shinikizo au msukumo wa damu na kuelezea daktari anavyopima presha.
Nini maana ya presha ya damu?
Neno la Kizungu ni
‘pressure’ (presha) au kwa Kiswahili shinikizo. Shinikizo la damu au
presha ni hali ya msukumo iliyomo kwenye damu. Kinachofanya damu itembee na kuzunguka mwilini ni presha yaani msukumo wa damu.....
Presha ni nguvu ya
msukumo au nguvu ya kusukuma. Mfano mzuri wa kuelezea maana ya presha ni
huu wa presha ya maji ya bomba. Kinachofanya maji yafike nyumbani kwetu
ni presha, ni msukumo wa maji. Kwa mfano huku kwetu Mbezi, asubuhi maji
yanatoka kwa presha kubwa sana. Ikifika saa 4 hivi presha inapungua na
ikifika saa 7 hakuna presha ya maji kabisa na maji hayatoki mpaka kesho
yake asubuhi yatakapotoka tena kwa presha kubwa sana.
Kuna njia nyingi za kujua
kuwa damu ina presha, ina msukumo au shinikizo. Damu ina presha
tukimaanisha inatoka kwa msukumo. Presha ni nguvu ya msukumo au nguvu ya
kusukuma. Ukijikata mshipa wa damu ambao ni mkubwa damu inatoka kwa
presha, kwa msukumo mkubwa, kwa shinikizo.
Makabila wanaotumia damu
kama chakula wana njia ya kupata damu kutoka kwa mnyama (ng’ombe) ili
kupata damu ya kumtengenezea chakula mama aliyejifungua. Wao wanajua
kuwa mama anahitaji chakula chenye damu ili naye ajitengenezee damu
mwilini ili kumrudishia damu aliyotumia wakati wa mimba na aliyopoteza
wakati wa kujifungua. Wazee wachungaji wanajua mshipa wa damu ambao
wakiutoboa hutoa damu kwa presha, kwa msukumo, kwa shinikizo na kupata
damu ya kutosha.
![]() |
Moyo unapampu damu mwilini
|
Daktari anapofanya
operesheni kubwa kwa mfano ya tumbo hukata mishipa ambayo mara ikikatwa
tu unaona damu inatoka kwa presha, kwa msukumo, kwa shinikizo.
Anachofanya msaidizi wake ni kuweka ‘presha’ juu ya mshipa uliokatwa na
kuzuia usitoe damu zaidi na huko daktari akitayarisha uzi wa kufunga huo
mshipa.
Mfano mzuri zaidi wa
kujua kuwa damu ina presha, ina shinikizo au msukumo ni unapomwona mtu
anatoa damu ya kuwasaidia wagonjwa au kama wewe mwenyewe umeishawahi
kutoa damu. Sindano inawekwa kwenye mshipa na hapo mara unaona damu
inaingia kwenye mpira ulioungana na hiyo sindano na kumiminikia kwenye
chupa. Presha, shinikizo au msukumo wa damu unaisukuma damu iende kwenye
chupa na baada ya muda kidogo unaona presha, msukumo wa damu, shinikizo
la damu limeishasukuma damu kutoka kwa Msamaria mwema na ameishatoa
nusu lita ya damu yake kuwasaidia wagonjwa.
![]() |
Presha ya damu inaisukuma damu painti moja hii kutoka kwa msamaria mwema kumpa mgonjwa
|
Presha ni mojawapo ya vipimo nyeti ambavyo hutumika kufuatilia (monitor) hali ya mgonjwa. Vipimo vingine nyeti ni hali ya joto mwilini (temperature), kupumua na mapigo
ya moyo (palsi). Presha huwa inabadilika badilika kutegemea na kama
umelala, umekula, unafanya mazoezi, ni mgonjwa, una msongamano wa mawazo
(stress), umesimama au umelala nakadhalika. Presha vile vile inapanda
jinsi umri unavyosogea.
Presha ina namba mbili: ya juu na ya chini. Ya juu ni wakati vyumba vikubwa vya moyo (vyumba vya chini) vinapopampu damu na kuielekeza mwilini. Ya chini ni
wakati moyo unapotulia kabla haujaendelea kupampu. Hii ni presha
iliyopo wakati wa katikati ya mapigo ya moyo. Kwa kuwa kipindi hicho
wakati moyo unapampu damu kinaitwa kwa kitaalamu ‘systole’ na kipindi
hicho wakati unapojilegeza kabla ya kupampu tena ‘diastole’ presha hizi
mbili zinaitwa ‘systolic’(sis-tolik) na ‘diatolic (daya-stolik). Kwa
hiyo presha inaripotiwa ya juu (systolic) na ya chini (diastolic) kama
120/80 (120 kwa 80). Mgonjwa atakuambia, “Nimepimwa presha na nimeambiwa
ni 120 kwa 80 yaani ‘systolic’ ilikuwa 120 na ‘diastolic’ ilikuwa 80”
Ni matumaini yangu kuwa
umeelewa maana ya presha na kuwa presha ina tarakimu mbili moja ikiitwa
‘systole’ na nyingine ‘diastole’. Wakati mwingine tutaelezea namna ya kupima
presha. usiache kutembelea Tovuti hii kila siku
0 comments:
Post a Comment