Leo tutajadili baadhi ya matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo, yaani Congenital Heart Disease.
Magonjwa ya moyo ya kuzaliwa nayo ni mengi, kuanzia yale
yanayosababishwa na matatizo madogomadogo ambayo kwa kawaida huwa
hayaonyeshi dalili au kuathiri maisha ya kawaida ya mtu, hadi yale
makubwa yanayohitaji kutibiwa kwa haraka.
Mara nyingi matatizo ya moyo ya kuzaliwa ni yale yanayozuia mtiririko
wa damu katika moyo au kwenye mishipa ya damu, au kusababisha damu
ipite njia nyingine isiyokuwa ya kawaida kwenye moyo.
Matatizo mengine ya moyo ya kuzaliwa lakini yasiyotokea sana ni pale
baadhi ya chemba za moyo zinapokosekana au badala ya kuwepo chemba mbili
mtoto huzaliwa na chemba moja ya ventricle au wakati mwingine upande wa
kulia au wa kushoto wa moyo huwa haujaumbika kwa ukamilifu hali ambayo
kitaalamu huitwa hypoplastic heart.
Miongoni mwa sababu zinazosababisha watoto kuzaliwa na matatizo ya
moyo ni pamoja na mmoja kati ya wazazi kuwa na tatizo la moyo la
kuzaliwa.
Iwapo mama alikuwa na tatizo la moyo la kuzaliwa kuna
uwezekano wa asilimia 2.5 hadi 18 wa kuzaa mtoto mwenye tatizo la moyo
pia. Iwapo baba alikuwa na tatizo la moyo la kuzaliwa uwezekano wa
kuzaliwa mtoto mwenye tatizo la moyo ni kuanzia asilimia 1.5 hadi 3.
Si kawaida mtoto zaidi ya mmoja kuzaliwa na tatizo la moyo katika
familia moja. Kuna uwezekano mtoto aliyeko tumboni wakati moyo
unapoumbwa akapatwa na maambukizi ya maradhi kama vile rubella, au
kuathiriwa na dawa anazotumia mama wakati wa ujauzito au sumu kama vile
lithium na hata pombe.
Yote hayo yanaweza kusababisha mtoto azaliwe na matatizo ya moyo.
Lakini pia baadhi ya matatizo ya jenetiki huambatana na matatizo kadhaa
ya moyo ya kuzaliwa. Matatizo hayo ya jenetiki kitaalamu huitwa Down’s
Syndrome, Digeorge syndrome na Turners Syndrome.
Jambo lingine linaloweza kusababisha mtoto azaliwe na matatizo ya
moyo ni pale mama anapokuwa na tatizo la kijenetiki linalojulikana kama
Phenylketonuria (PKU).
Hali hiyo hutokea wakati mwili unaposhindwa
kuyeyusha sehemu ya protini inayoitwa phenylalanine (Phe).
Phenylalanine kwa kawaida hupatikana katika kila chakula lakini
kiwango chake kinapokuwa juu mwilini huweza kuharibu ubongo na
kusababisha mtindio wa ubongo.
Baadhi ya wajawazito hupata tatizo hilo
ambalo huzidisha uwezekano wa mtoto kuzaliwa akiwa na matatizo ya moyo
na ya ubongo pia.
Tuesday, 28 October 2014
- Blogger Comments
- Facebook Comments
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment