-

-

-

-

-

Habari Mpya

Tuesday 28 October 2014

Kisukari kinavyosababisha upofu wa kudumu.

Lawrence Mashati (si jina lake halisi), anahudhuria kliniki ya ugonjwa wa kisukari katika moja ya hospitali binafsi jijini. 

Ugonjwa ambao unamsumbua kwa miaka kadhaa sasa.
Amepata matibabu kulingana na maelekezo ya madaktari na wauguzi katika kliniki hiyo. 
Hata hivyo, katika hali ambayo anaona si ya kawaida, uwezo wake wa kuona unapungua.

Tofauti na miezi kadhaa nyuma, hivi sasa hata kuweka vocha katika simu yake hawezi tena. Sasa inabidi amuombe mtu mwingine amsaidie.

Mbaya zaidi hata ukubwa wa maandishi anayotumia katika kompyuta yake anayofanyia kazi ameyarekebisha na sasa ni makubwa zaidi tofauti na awali. Hajui tatizo hilo linatokana na nini.

Mashati ni mmoja kati ya watu milioni 346 ulimwenguni wanaougua ugonjwa wa kisukari ambao ni sawa na asilimia 6.4 ya watu wote. Kati ya hao, asilimia 80 wanatoka katika nchi zinazoendelea, Tanzania ikiwa miongoni mwake.

Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inabainisha kuwa hapa nchini, kati ya watu 10, watatu wana kisukari na ugonjwa huo umesababisha upofu kwa asilimia 4.8 ya wagonjwa wote nchini.


Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Sayansi ya Afya Muhimbili (Muhas) na daktari bingwa wa magonjwa ya macho katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dk John Kisimbi anasema upofu unaotokana na kisukari ni tatizo linalozidi kukua.

Anasema wagonjwa wengi wa kisukari wapo katika hatari ya kupata upofu wa kudumu kutokana na kushindwa kuhudhuria kliniki ya macho kujua athari za kisukari katika mfumo wa kuona.

Kisukari ni nini?

Anasema sukari inahitajika kwa ajili ya ustawi wa mwili wa binadamu na kwa kawaida, mfumo ndiyo ambao unaruhusu kuwapo kwa kiwango kinachohitajika mwilini.
Anasema ugonjwa wa kisukari unatokana na hitilafu katika mfumo mzima wa kudhibiti kiwango cha sukari mwilini.

Daktari huyo anasema katika mwili wa binadamu, sukari inahitajika kwani baada ya kuchomwa mwilini ndipo hutoka nguvu ambayo kufanya kazi mbalimbali sanjari na kupumua. Anasema chakula anachokula binadamu kwa kawaida hufyonzwa katika utumbo na kiasi cha sukari kinachohitajika hubaki mwilini baada ya kukutana na vimeng’enyo au kwa jina jingine insulini, kutoka katika kongosho.

“Kiasi kinachobaki kinaweza kuhifadhiwa ama katika ini au mafuta mwilini,” anasema na kuongeza kuwa mfumo unapopata hitilafu ndipo linapozuka tatizo la ongezeko la sukari katika damu.

Anasema hitilafu hizo ni pamoja na kongosho kushindwa kuzalisha vimeng’enyo vya kutosha kwa ajili ya kazi iliyokusudiwa au vilainishi hivyo kushindwa kufanya kazi ipasavyo.

Dk Kisimbi anasema, sukari inahitajika kwa ajili ya ustawi wa mwili wa binadamu na kwa kawaida mfumo ndiyo ambao unaruhusu kuwapo kwa kiwango kinachohitajika.

Anasema mfumo unaposhindwa kuhakikisha sukari ipo mwilini kwa kiwango kinachohitajika, inasababisha uwepo wa sukari nyingi kuliko inavyotakiwa kwenye mzunguko wa damu.

Upofu

Dk Masimbi anasema mgonjwa anaweza kupata upofu kwa namna mbili tofauti. Anabainisha kuwa upofu unaweza ukajitokeza katika mishipa midogo iliyopo nyuma ya retina ya jicho.

Anasema mishipa hiyo midogo, huvujisha protini na majimaji kutoka katika damu na hujikusanya pembeni mwa mishipa na kuonekana kama chembechembe nyeupe.

Kutokana na hali hiyo baadaye mishipa huziba na sehemu ya retina inashindwa kupata damu na wakati mwingine hupasuka na kuvuja damu.

“Kadiri muda unavyokwenda sehemu nyingi zaidi zinavuja lakini ni ndani tu ya retina na siyo katika ute na hali hiyo isipodhibitiwa huzalisha mishipa mipya kwa ajili ya kuzalisha damu,” anasema.

Mshipa hiyo mipya isiyo imara hujaa katika chumba cha ute na damu huvuja na kujaza chumba hicho na ndipo jicho linapoziba kabisa na kumfanya mhusika awe na upofu wa kudumu.

Daktari huyo anasema hali hiyo pia huleta athari katika figo, miguu, ubongo, moyo na ini.

Pia husababisha wenye tatizo hilo kushindwa kusoma, kuona maandishi, kuwatambua watu na hufika wakati anakuwa hawezi kumtambua mtu ambaye anamfahamu hadi afike karibu naye. “Anakuwa kama anaona kivuli na si taswira halisi na hali hiyo hufanya seli ambazo zingeweza kutafsiri taswira iliyopo mbele yake kushindwa kufanya kazi,” anasema.

Daktari huyo anasema athari hizo zinaweza kujitokeza mapema kabla mishipa ya pembeni haijaota au sambamba na uotaji wake na hatimaye kuvuta damu kwenye ute.

“Asilimia kubwa ya wagonjwa wa kisukari hawahudhurii kliniki ya macho ili kutambua kiwango cha athari zinazotokana na ugonjwa huo katika uwezo wa kuona,” anasema.

Anasema uono hafifu hadi upofu wa kudumu kwa mgonjwa wa kisukari ni jambo ambalo linaanza taratibu na kama asipolibaini mapema, anakuwa katika hatari ya kupata upofu wa kudumu.

Takwimu zinaonyesha kwamba idadi ya watu wenye ugonjwa wa kisukari Afrika inatarajiwa kuongezeka mara mbili katika kipindi cha miaka 20 ijayo.

Shirikisho la Kimataifa la Kisukari (IDF), linasema kwamba inakadiriwa watu milioni 371 hivi sasa wanaishi na ugonjwa huo unaotokana na mwili kushindwa kutengeneza viwango vya sukari katika mfumo wa damu.

Kulingana na ripoti ya karibuni ya Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa (WHO), idadi hiyo inazidi kukua hasa katika nchi zinazoendelea ambako watu wengi wamekuwa na uzito kupita kiasi huku wakiwa hawafanyi mazoezi ili kuuweka mwili sawa.

Tatizo la sukari lisipodhibitiwa husababisha upofu, figo kushindwa kufanya kazi, ulemavu wa viungo na hata kifo.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

0 comments:

Post a Comment

Item Reviewed: Kisukari kinavyosababisha upofu wa kudumu. Description: Rating: 5 Reviewed By: Unknown
Scroll to Top