-

-

-

-

-

Habari Mpya

Wednesday 29 October 2014

Unazijua Sababu za asali kuwa salama ijapo inatoka kwenye mazingira hatari.

afya tele
Katika tathmini ya haraka ya wadudu ambao wanaweza wakaeneza maradhi mbalimbali ukiacha nzi, nyuki anaweza kuwa mmojawapo.
Kama ilivyo nzi, nyuki hutua maeneo mbalimbali kutafuta malighafi kwa ajili ya kutengeneza asali. Katika harakati hizo nyuki hutua maeneo mengi kuchukua vitu muhimu kwa ajili ya kutengeneza asali.
Ingawa nzi anatembea maeneo machafu, wanasayansi wanasema hata maeneo ambayo nyuki anatembelea kutafuta vitu kwa masilahi yake, kuna vimelea vya maradhi mengi ambayo yanaweza kumdhuru yeye na hata binadamu wanapotumia asali.
Kwa sababu hiyo, wanasayansi wanasema hata nyuki yupo kwenye mazingira ya kusambaza maradhi ingawa asali yake imekuwa ikitumiwa na binadamu tangu maelfu ya miaka iliyopita.
Lakini swali likaja, je asali ina vimelea vya magonjwa? Hapo jibu likawa ni kuchunguza kama inaweza ikawa chanzo cha maradhi pale binadamu anapoitumia.
Wakiwa maabara wakachunguza asali kwa kina na kubaini kuwa haina aina yoyote ya kimelea hai ambacho ni hatari kwa afya.
 Ikabidi wajiulize, kulikoni, wakati wanajua kuwa mazingira ambayo anapita nyuki si salama; yana vijidudu wengi hatari?
Kulikuwa na mawazo kwamba huenda nyuki ana namna yake ya kuchukua vitu katika maeneo anayopita ili asibebe bakteria, fangasi au virusi ambao ni hatari kutokana na kuwa ni chanzo cha maradhi.
Walipomchunguza wakaona kuwa nyuki wala hana namna ya ajabu anayofanya. Waliona anaingia kwenye maua hata yale ambayo yana bakteria au virusi hatari, akabeba ungaunga na umajimaji ulio na sukari kwenye maua na kuondoka nao.
Kwa kuchunguza hilo ilionekana haiwezekani kwa namna ambayo nyuki anachukua mali ghafi zake angeweza kubagua vimelea hatari vya magonjwa.
Waswidi wategua kitendawili
Wanasayansi wa Sweden wiki hii wamekuja na kile walichosema ni kubaini kile anachofanya nyuki ili asali isiwe na vimelea hatari vya magonjwa.
Katika ugunduzi wao wanasema unaweza ukasaidia fani ya sayansi ya afya juu ya namna ya kutengeneza dawa za kukabili maradhi mbalimbali yanayoenezwa na bakteria.
Kumbuka magonjwa mengi, yanayosumbua binadamu yanatokana na jamii ya bakteria wanaopatikana katika mazingira mbalimbali yanayomzunguka binadamu.
Wanasayansi hao wa Chuo Kikuu cha Lund nchini Sweden wamenukuliwa na Shirika la Utangazaji la BBC wakisema wamebaini kuwa katika tumbo la nyuki kuna kemikali ambazo zinatumika katika kuua aina yoyote ya bakteria hatari.
Tena wakasema kemikali hiyo huzalishwa na aina nyingine ya bakteria ambao hawa hukaa ndani ya tumbo la nyuki na kazi yake hiyo ni kutoa kemikali za kuua vimelea wowote hatari.
Kemikali inayotolewa na bakteria hai ni aina 13 za asidi zinazofanana na zile zinazopatikana kwenye maziwa.
Aina hizo 13 za asidi wamezielezea kuwa zimetengenezwa kwa kanuni maalumu ambayo inaua aina nyingi za bakteria wa maradhi.
“Tunaweza kutumia kanuni ya ina hiyo kusaidia kutengeneza dawa ambayo haitamuathiri binadamu bali aina nyingi za bakteria hatari kwa afya ya binadamu,” anasema Dk Tobias Olofsson, mtaalamu wa Kitengo cha Tiba za Maradhi yaenezwayo na vimelea wa Chuo Kikuu cha Lund.
Uzuri wa bakteria hao waliopo kwenye tumbo la nyuki, anaeleza, ni uwezo wao wa kuchunguza aina ya kimelea hatari na kutengeneza sumu inayofaa kumuua.
Kulingana na maelezo ya Dk Olofsson, bakteria hao ni sawa na kiwanda cha silaha ambacho kina wafanyakazi mahiri ambao wakiona tu aina ya adui, wanamtambua na mara moja wanaunda silaha ya itakayotumika kumuangamiza kulingana na umbile lake na maarifa yake katika kujihami.
“Inaonekana kuwa mtindo huo kwa nyuki umedumu kwa mamilioni ya miaka na ndiyo maana nyuki hawadhuriki kiafya na asali wanayotengeneza ni salama pia kwa afya ya binadamu kwa sababu haina vimelea wa maradhi,” anasema mtaalamu huyo.
Kwa njia hiyo anasema asali ya nyuki huweza kubakia kwa muda ikiwa hai kwa maana ya kwamba kutoweza kuingiliwa na bakteria hatari kiafya.

 Namna asili inavyotengenezwa
Nyuki anaanza kutengeneza kwa kutembelea maua ili kukusanya mali ghafi za kutengeneza asali.
Kwa kawaida nyuki huvutwa na aina fulani ya umajimaji kwenye maua ijulikanayo kama nectar ambao huvutia wanyama ambao katika kuyavuna hujikuta wanausaidia kupevusha.
Upevushaji huo unatokana na kusaidia poleni – mbegu za kiume ambazo zipo katika hali ya unga na kumwagika kwenye ovary – sehemu ya kike ya ua.
Wakati wa kutengeneza asali, nyuki hutoa vimeng’enyo kadhaa ambavyo katika hatua tofauti hufanikiwa kugeuza sukari iliyopo kwenye nectar kuwa sucrose, glukosi na fructose na baadaye ni gluconic ambayo ni asali.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

0 comments:

Post a Comment

Item Reviewed: Unazijua Sababu za asali kuwa salama ijapo inatoka kwenye mazingira hatari. Description: sababu za asali kuwa salama ijapo inatoka kwenye mazingira hatari Rating: 5 Reviewed By: Unknown
Scroll to Top