-

-

-

-

-

Habari Mpya

Monday 17 November 2014

KISUKARI; Kisukari cha mimba ni ugonjwa unaokua kwa kasi SANA

Ugonjwa huu unatajwa kuwapata wanawake wakati wa ujauzito, pasipo wao wenyewe kujua na matokeo yake hujifungua watoto wenye uzito mkubwa, walio na matatizo ya kimaumbile na wengine huzaliwa wakiwa na rangi ya manjano.


Idadi kubwa ya wanawake nchini inaelezwa kuugua ugonjwa wa kisukari cha mimba kitaalamu ukijulikana kwa jina la’Gestestional Diabetes’.
Ugonjwa huu unatajwa kuwapata wanawake wakati wa ujauzito, pasipo wao wenyewe kujua na matokeo yake hujifungua watoto wenye uzito mkubwa, walio na matatizo ya kimaumbile na wengine huzaliwa wakiwa na rangi ya manjano.
Wataalamu wanaeleza kuwa ugonjwa huo unashika kasi duniani na kwamba wanawake wajawazito, ambao huongezeka uzito kwa kasi katika miezi mitatu ya mwanzo ya ujauzito wao, wanakabiliwa na hatari zaidi ya kupata kisukari cha mimba.
Katika mahojiano maalumu na Mwananchi Jumamosi, Mkuu wa Idara ya Kisukari katika Hospitali ya Taifa Muhimbili(MNH) ambaye pia ni Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Kisukari, Dk Mohammed J Mohammed anasema kuwa ugonjwa huo huwapata kinamama hao hasa kipindi cha miezi sita au zaidi ya ujauzito.
“Kisukari cha mimba humpata mwanamke kipindi cha ujauzito hasa katika kipindi cha mwisho kuanzia wiki ya 24 na kuendelea. Kisukari hiki hakidumu kwa muda mrefu kwani kinaweza kupotea mara tu baada ya mama kujifungua, lakini pia kinaweza kuendelea na hapo tunasema kimebadilika kuelekea katika hatua nyingine,” anasema Dk Mohammed.
Anasema kuwa idadi kubwa ya wanawake hawafanyi vipimo vya kisukari cha mimba wanaokuwa wajawazito mijini na vijijini hivyo kutojua hali zao kiafya na kama wapo katika hatari ya kupata kisukari cha mimba.
“idadi kubwa ya wanawake hawafanyi vipimo, hawa hujifungua bila kujua wana tattizo hilo hatima yake linaisha. Lakini wapo pia ambao huendelea na tatizo hilo na baadaye linakuwa kubwa.”
Uchunguzi mpya unaonyesha kuwa wajawazito watakaoongeza uzito wa gramu 403.70 kwa wiki, wako katika hatari zaidi ya kupata kisukari cha mimba ikilinganishwa na watakaoongeza uzito wa chini ya gramu 272.15 kwa wiki.
Sababu za kisukari cha mimba
Dk Mohammed anasema: “Kila binadamu ana mfumo wa sukari mwilini mwake na inahitajika, lakini inategemea sukari ile inaingia kwa kiasi gani mwilini na matumizi yake. Kupendelea kula vyakula vyenye sukari kwa wingi ikiwemo soda na vyakula vingine vyenye kuongeza sukari mwilini kunasababisha kongosho kuchoshwa, lakini pia kuna sababu zinginezo.”
Anaeleza kuwa wakati mwingine ni usugu wa homoni kutumia chembe hai na hii hutokea kwa watu wenye uzito mkubwa kwani homoni ile inakuwa imezungukwa na mafuta. Pia husababisha ongezeko la baadhi ya vichocheo kama Progesterone, Estrogen na free Cortisol vinavyoongeza kiwango cha sukari katika damu.
Wakati huohuo kichocheo cha Human Placental Lactogen huzuia insulin kufanya kazi kwa ufanisi, hivyo kusababisha kiwango cha insulin kuongezeka katika damu.


Dk Mohamed anafafanua kwamba, mwili unaposhindwa kutengeneza insulin ya kutosha kupambana na ongezeko la sukari katika damu, kisukari cha mimba hutokea, mara nyingi hutokea mimba ikiwa na umri wa miezi mitano au zaidi na kwa kawaida huisha wiki sita baada ya mwanamke kujifungua.
Dalili zake
Kisukari cha mimba kina dalili kadhaa, lakini kwa kawaida huainishwa kwa vipimo (screening), vinavyochukuliwa wakati wa ujauzito.
Kwa mujibu wa Dk Mohammed dalili za kisukari cha mimba ni chache na mara nyingi hazionekani kwa uharaka zaidi ya kujitokeza baada ya kujifungua, hivyo kuwashauri wajawazito kupima kisukari mara kwa mara.
Anasema kuwa mwanamke anashauriwa kupima kisukari kabla ya ujauzito, anapokuwa mjamzito na baada ya ujauzito.
Mtaalamu huyo anabainisha kuwa kupimwa kwa tatizo hilo husaidia mama kuanza matibabu mapema na kuondoa sukari iliyojaa katika kondo.
Anataja dalili za mwanamke mwenye kisukari cha mimba kuwa ni kuongezeka uzito siku za mwanzoni mwa mimba, kuwepo historia ya kuwa na kisukari katika familia, kuwahi kujifungua mtoto mwenye uzito mkubwa na mimba kuharibika mara kwa mara.
Nyingine ni historia ya kisukari cha mimba, mkojo kuwa na sukari mara kwa mara, kuzaa mtoto mfu, uzito au unene uliokithiri, shinikizo kubwa la damu la muda mrefu au umri zaidi ya miaka 35.

Matibabu yake
Dk Mohamed anasema kuwa aina hii ya kisukari huchomoza wakati wa mimba, na ili kulinda mtoto tumboni mara nyingi inabidi mja mzito apewe insulin ili sukari iliyo katika damu iwe kati ya 4-8mmol/l.
Anabainisha kwamba ikwa mwanamke atakuwa na sukari nyingi kwenye damu yake akiwa na mimba, kutakuwa na uwezekano mkubwa kwamba, mtoto atazaliwa na athari tofauti au uzito uliopitiliza.
Baada ya kugundulika na kisukari cha mimba, mama hushauriwa kutumia vyakula vya sukari visivyofyonzwa kwa uharaka kama soda na juice, badala yake atumie matunda halisi yatakayomsaidia sukari yake kutopanda kwa uharaka na pia nyuzinyuzi za matunda zitamsaidia katika mmeng’enyo mzuri wa chakula. Daktari bingwa huyo anaeleza kwamba mama atapewa dawa aina za insulin ni chembechembe, lakini kama pia atakataa hizo, hupatiwa dawa za vidonge na huyu atalazimika kupima sukari yake mara kwa mara.

Athari zitokanazo na ugonjwa huu
DK Mohamed anabainisha kuwa kuna hatari inayoweza kumpata mtoto atakapozaliwa ambayo ni kifo iwapo sukari yake itashuka kwa kasi, ndio maana mtoto mkubwa anapozaliwa hupewa glucose ili aendelee kupata ile sukari kwa kipindi fulani. Pia mtoto anaweza kuzaliwa na matatizo ya kimaumbile, kuzaliwa na rangi ya manjano.
Mama anaweza kupata athari za kushindwa kujifungua kwa njia ya kawaida kwa kuwa mtoto atakuwa na uzito wa juu sana.
Asilimia 4 ya kina mama ambao watapata kisukari wakati wa ujauzito wanakabiliwa na hatari ya kupata ugonjwa wa kisukari baadaye maishani mwao, hiyo ikiwa ni pamoja na watoto wao.
Mtoto kuzaliwa na uzito wa juu mtoto mwenye afya anatakiwa kuzaliwa na uzito kuanzia kilogram 2.5 hadi kilogram 4 akizidi zaidi ya hapo hilo ni tatizo jingine. Mtoto anapozaliwa na uzito mkubwa mara nyingi huwa na njaa sana ndio maana hupewa nyongeza ya glucose na atakuwa anakula sana kwa kuwa alikuwa akipata sukari hiyo alipokuwa tumboni. Dk Mohammed anabainisha kuwa kondo analokaa mtoto hujitengenezea sukari nyingi na hivyo kupelekea mtoto aliyemo ndani kuitumia sukari hiyo inayomfanya azidi kukua siku baada ya siku. Anasema mtoto atakapokuwa anakula sukari hiyo moja kwa moja mwili wake unazidi kutengeneza mafuta kwa wingi.
Anasema tatizo hili pia linawapata zaidi watu wa makabila ya Afrika, Wamarekani Weusi, Afrocaribeans, Hispania, nchi za Pacific na Kusini mwa bara la Ulaya.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

0 comments:

Post a Comment

Item Reviewed: KISUKARI; Kisukari cha mimba ni ugonjwa unaokua kwa kasi SANA Description: Rating: 5 Reviewed By: Unknown
Scroll to Top