-

-

-

-

-

Habari Mpya

Friday 14 November 2014

VIATU HATARI KWA AFYA YA WANAWAKE.


‘Mchuchumio’ ama viatu vyenye visigino virefu, ni mojawapo ya vitu vinavyopendwa na baadhi ya wanawake mbalimbali, si katika Tanzania bali dunia nzima.

Wataalamu wanaeleza kuwa viatu hivi huharibu pingili za uti wa mgongo na huvunjavunja mifupa ya visigino.
Wanawake wenye maumbo ya kati, ambao si wanene wala wembamba wamekuwa wakipendelea viatu virefu.
Kwa kiasi kikubwa wasichana wafupi, wamekuwa wakipendelea kuvaa viatu virefu ili angalau na wao waonekane warefu.

Ashura Mgweno, mfanyakazi wa Kampuni ya Usafi jijini Dar es Salaam, anasema: “Nimetumia viatu kwa muda mrefu, lakini sasa sitaki kusikia viatu virefu. Mimi ni mfupi, nilikuwa navaa sana, lakini sasa sitaki hata kuviona jinsi vilivyonitesa,” anasema.

Anasema kuwa viatu virefu muda wake ni miaka mitatu, inaharibu visigino na misuli ya miguu na kutengeneza vigimbi ambavyo baadaye husababisha maumivu makali.
Akizungumzia hili, Ruth Erasto ambaye anafanya kazi katika ofisi moja jijini Dar es Salaam, anasema aliacha kuvaa ‘mchuchumio’ kwa maagizo ya daktari.

“Niligawa viatu vyangu vyote virefu baada ya kupatwa na maumivu ya mgongo. Viatu virefu havilinganishi mwili wakati wa kutembea na niliagizwa na daktari kuachana na viatu virefu…hiyo ilitokana na mimi kuanza kupatwa na matatizo ya mgongo,” anasema.
Anasema kuwa alipatwa na matatizo hayo bila kufahamu, lakini baada ya kuchunguzwa, ndipo ikabainika kupatwa na matatizo hayo.

Mwanamama mwingine aliyepatwa na matatizo hayo, Victoria, anasema kuwa inamlazimu kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kila mara kwa ajili ya kuangaliwa maendeleo ya mgongo baada ya kuvaa viatu virefu kwa muda mrefu na kumletea athari hizo.
Victoria ambaye ni mfupi na mnene kiasi kwa umbile, anasema kuwa pamoja na kupenda kuvaa viatu hivyo, hataki kusikia habari zake.
“Nakuambia sina hamu na viatu hivi, acha kabisa, nimekoma…nimekwenda Muhimbili hadi nimechoka, maumivu kuanzia kiuno hadi mgongo,” anasema.


Jozi mbili
Hakika, wapo wanawake wanaofahamu madhara ya kuvaa viatu hivyo, lakini wengine wanafahamu, lakini wanapuuza. Baadhi ya wanaopuuza ni kutaka kuonekana wa kisasa zaidi, licha ya kuwa wanahisi maumivu makali wanapovaa.
Mara kwa mara, wengi wa wanawake hulazimika kubeba viatu jozi zaidi ya moja, vile vya chini (flat shoes) kwa ajili ya kubadilisha pindi mambo yanapokuwa magumu.

Christina Mdete, Mkazi wa Yombo Buza, Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam anasema amekuwa akibeba jozi mbili za viatu anapotoka nyumbani na kuvaa viatu virefu anapoingia ofisini. “Hata ninapokuwa ofisini, navua kisha navaa ‘flat’…ah! siwezi wewe, kutwa nzima, vinaumiza halafu hauko na raha ukivaa muda wote.

Anasema hata wanaokwenda kwenye sherehe, hutumia muda mfupi kuvaa, kwani ni pale wanapokwenda kutoa zawadi na baada ya hapo, vinavuliwa na kuvaliwa viatu vya chini.
Wasichana wengi wanafahamu ‘mchuchumio’ husababisha maumivu makali lakini je, ndiyo kutimiza usemi wa ukitaka uzuri shurti udhurike? Kwa kawaida, urembo hauwezi kusababisha maumivu, lakini kuvaa viatu virefu kuna athari kubwa.

Utafiti mbalimbali wa hivi karibuni unaonyesha kuwa viatu virefu havifai hata kidogo. Kimsingi, uvaaji wa viatu virefu husababisha maumivu makali ya misuli ya miguu pamoja na nyama za nyuma kwenye maungio ya magoti na enka.

Uharibifu ni mkubwa pia huweza kutokea ndani ya magoti kwa kuhamisha maungio (dislocate). Kwa jinsi mhusika anapovaa viatu virefu kwa muda mrefu, ndipo inaposababisha madhara ya muda mrefu.
Mbali na hayo, vilevile, husababisha mwili kukosa usawa wakati wa kutembea, misuli ya miguu kubana, kupoteza mwelekeo wa mwendo halisi na wakati mwingine husababisha mhusika kuanguka na kumsababishia maumivu makali.
Madaktari wanashauri kuvaa viatu virefu kuwe kwa muda maalumu kwa shughuli maalumu na visizidi urefu wa inchi mbili.

Kama mtu alizoea kuvaa viatu virefu kwa muda mrefu, inashauriwa kuacha taratibu badala ya kubadilika haraka kwenda kwenye viatu. Kama viatu virefu vitavaliwa kazini, ni vizuri kuwepo na viatu vingine vya kubadilisha.

Utafiti mwingine unaonyesha kuwa viatu virefu husababisha maumivu makali ya dole gumba la mguu, kuzuia ukuaji wa kucha na matatizo mengine.

Watafiti hao wa Chuo Kikuu cha Griffith kwenye mji wa Queensland, Australia wakiongozwa na Dk Neil Cronin, katika utafiti wao, waliliambia gazeti la New York Times kwamba wanaendelea kufanya utafiti kuona madhara zaidi yanayoweza kupatika.

Katika uchunguzi uliochapishwa kwenye jarida la Journal of Applied Physiology, Dk Cronin anasema wanawake wengi waliofanyiwa utafiti wamebainika kutokuwa imara katika miguu yao, kupatwa na maumivu makali na kuharibiwa misuli na enka ya mguu.

Naye Dk Orly Avitzur, Mganga Mshauri kwenye kitongoji cha Tarrytown, New York, Marekani anasema kuwa alifanya utafiti kwa wanawake wa zaidi ya miaka 40 kuwa hawawezi kuvaa viatu virefu kwa kuwa miguu yao tayari imeharibiwa.

“Kama ni miaka 20 sawa, ni kitu kingine,” Avitzur anasema. “Kama ikiwa ni zaidi ya miaka 40 ni tatizo na itakuwa suala lingine mtu akivaa viatu hivyo, lakini chini ya hapo haina shida sana.”
Mtaalamu wa Mifupa katika Hospitali ya TMJ, Dar es Salaam, Dk Edemeza Machange anasema kuwa matatizo ni makubwa kwa mtumiaji wa viatu virefu na athari zaidi huwakumba wanawake wanene.

“Ni mbaya sana…kwa wanawake wanene haishauriwi watumie viatu virefu kwa kuwa vitawaletea matatizo mengi katika miili yao,” anasema.
Kama walivyosema wataalamu waliotangulia, Machange anasema kuwa kubwa linaloumiza wanawake wengi ni kuvaa viatu virefu kwa kipindi kirefu na matokeo yake ni kuumwa mgongo kwani uharibu mpangilio wa pingili za uti wa mgongo.

“Kwa kawaida mtu anapoteza mwendo halisi, sasa kutotembea kwa mpangilio, huharibu mfumo wa pingili za mgongo, hata kiuno na kusababisha maumivu makali…tumekataza wengi kuvaa viatu virefu baada ya kupatwa na matatizo ya mgongo.”

Anawashauri kinamama hasa wasichana, wafahamu kuwa pamoja na kutaka urembo, lazima wajali afya zao kwa kuvaa viatu virefu katika kipindi kifupi na zaidi ni kuangalia madhara kwa baadaye kuliko kukimbilia kuvaa viatu virefu kwa ajili ya urembo.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

0 comments:

Post a Comment

Item Reviewed: VIATU HATARI KWA AFYA YA WANAWAKE. Description: Rating: 5 Reviewed By: Unknown
Scroll to Top