-

-

-

-

-

Habari Mpya

Tuesday, 29 July 2014

LISHE BORA YA MTOTO KUANZIA MIEZI 12-18






Kuanzia miezi 12 watoto wengi huwa wameanza kutembea na hivyo kuongeza michezo. Kutokana na kucheza zaidi watoto wanahitaji kula vizuri ili kuendeleza uzito na afya zao. Pia watoto wanakuwa wameota meno angalau nane hivyo wanaweza kutafuta chakula kilichopondwapondwa. Katika umri huu mtoto anaweza kula chakula chochote ambacho hana allergy nacho.



Ni vyema ukaandaa ratiba ya kumlisha mtoto wako na menu ya nini cha kumpa kila siku. Ratiba iwe mahali ambapo kila mtu anaweza kuiona kwa urahisi ili wote wanaohusika na malezi ya mtoto wajue nini mtoto anatakiwa kula na wakati gani. Kila siku hakikisha mtoto anapata vyakula kutoka kwenye makundi makuu ya vyakula; wanga, vitamini, protini na mafuta.




Vyakula kulingana na makundi haya ni kama ifuatavyo:

Wanga

•         Nafaka

•         Viazi

•         Ndizi za kupika

Protini

•         Nyama (Ng’ombe, Kuku, Mbuzi n.k)

•         Samaki

•         Mayai

•         Maziwa

•         Maharage na jamii yake



Vitamini

•         Mboga za majani

•         Matunda

•         Mafuta

•         Karanga

•         Ufuta

•         Siagi

Vyakula hivi vinaandaliwa kwa namna mbalimbali ili kuweza kuliwa  vizzuri na watoto. Nafaka kama mahindi, mtama, ulezi, mchele n.k unasaga unga kwa ajili ya kumpikia uji. Kwa sababu mtoto ameshakuwa kidogo ni vyema ukamsagia lishe (kuchanganya nafaka mbili au tatu pamoja na karanga au ufuta). Karanga unaweza saga ppamoja na nafaka au ukasaga mwenyewe kwenye mashine na kumwekea kiasi kila unapopika chakula chake. Viazi na ndizi hutumika zaidi kupikia mtori ukichanganya na vyakula vya protini (nyama, samaki, maziwa) na mbogamboga, vile vile unaweza weka kiasi kidogo cha njegere.



Protini (nyama, samaki) unachemsha vizuri na kumpa supu nzito isiyo na viungo vingi. Samaki tumia wale wakubwa wasio na miiba midogo midogo. Mayai unachemsha na kumpa kiini ukichanyanya na maziwa kidogo au unapikia yai kwenye uji. Mtoto wa umri huu hatakiwi kula zaidi ya mayai matatu ya kienyeji kwa wiki, usimpe mayai ya kisasa kabisa. Maziwa unamchemshia ya kunywa na vilevile unapikia kwenye chakula chake, usipike chakula bila kuweka maziwa fresh. Unaweza pia chukua wali uliopikwa, ukachemsha maziwa nakisha kusaga wali na maziwa kwenye blender na kumpa mtoto. Wali unaweza upika na karoti ili kuongeza virutubisho. Supu ya maharage yaliyochemshwa tu ukasaga kwenye blender na maharage kidogo ina virutubisho pia kwa ajili ya mtoto wako.



Vitamini mbalimbali zinapatikana kwenye mboga za majani na matunda. Mpikie  mboga na kumsagia kwenye blender na kumpa kama supu, au changanya aina moja ya mboga kidogo tu kwenye mtori wake nakusaga kwenye blender. Matunda hakikisha yanaandaliwa kwa usafi wa hali ya juu, saga kwenye blender na umpe kama uji mzito. Matunda kama papai, parachichi na ndizi mbivu sio lazima umsagie ila hakikisha unapondaponda. Unaweza kumtengenezea juice ila matunda bila maji ni mazuri zaidi. Mkamulie chungwa mara moja kwa wiki, machungwa yana asidi hivyo usimpe kwa wingi.



Usisahau kumpa maji ya kunywa yaliyosafi na salama. Usimpe soda wala juisi za kununua madukani, hazina thamani yoyote kiafya na kemikali zilizotumika hazifai kwa mtoto.

  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

0 comments:

Post a Comment

Item Reviewed: LISHE BORA YA MTOTO KUANZIA MIEZI 12-18 Description: Rating: 5 Reviewed By: Unknown
Scroll to Top