1. Stori ya Yohane:
Nimekuwa na
matatizo ya homa za mara kwa mara, kikohozi kikavu na ukurutu kwenye
ngozi. Nilihisi labda nimeishaambukizwa VVU. Mwanzo wa mwaka huu
nilijisikia kudhoofika sana. January 25 nilienda kupima nikaambiwa nina maambukizi ya VVU. Walinipima CD4 wakakuta zimeishapungua sana na ziko 100 tu.
Nilijisikia
vibaya sana. Niliomba Mungu nifie mle kliniki nilikoenda kupima lakini
sikufa. Nilitoka mle nimechanganyikiwa. Nilikuwa nalia nikisema,
“Nitamwambiaje mke wangu kuwa nina UKIMWI. Nitamwambiaje kuwa
nimeishaambukizwa na kumwambukiza VVU? Nilipokuwa
njiani naenda nyumbani niliomba nigongwe na gari lakini magari yalikuwa
yananikwepa, hayapendi kunigonga. Hakuna aliyetaka kunigonga. Nilifika
nyumbani, nikampigia magoti mke wangu na kumlilia nikimwambia, “Nisamehe mke wangu nina UKIMWI.” Sikuthubutu kusema, “Nimekuambukiza.” Nilimwambia tu, “Nisamehe nina UKIMWI.”
Mke wangu
alisikitika na kusema, “Mume wangu, umetuua, tutakufa. Mimi nimekuwa
mwaminifu kwako miaka yote hii; kumbe wewe ulikuwa unatembea nje huko.”
Niliomba ardhi ipasuke inimeze lakini naona Mungu alikuwa ameishaamua
kuwa ni lazima niteseke kwa muda mrefu.
Kesho yake mke wangu alienda kupima na kwa muujiza ambao mpaka sasa sijaelewa, alikutwa hajaambukizwa.....
Sasa
imeishapita miezi mitatu natumia dawa za kurefusha maisha. Najisikia
afadhali. Kinachonipa nguvu ni sapoti ninayopata kutoka kwa mke wangu,
wazazi na ndugu zangu. Wamelichukulia hiji jambo kwa kunionea huruma.
Wazazi na ndugu zangu hufika mara nyingi nyumbani na kukaa na sisi na
kutufariji. Nina bahati kuwa nimepata janga hili miaka hii ya karne hii.
Kama ingekuwa karne iliyopita, wagonjwa kama mimi walikuwa wanatengwa
na kukimbiwa na familia zao na kuwaacha wafe haraka. Sasa napewa dawa,
napewa sapoti na mke wangu, wazazi na ndugu zangu. Mke wangu bado
ananichukulia kama mume wake na ndugu zangu kama ndugu yao.
Nilipougua kilichonisikitisha sana ni kufikiri kuwa nitakufa kabla ya mama yaani mama atanizika. Nilianza kufikiria jinsi mama atakavyosikitika kunizika. Ninajua sasa kuwa kama nikijitahidi kujizatiti kimwili na kimawazo nitapata afya ya kuweza kuishi na kumzika mama kuliko yeye anizike mimi. Kujitahidi kutumia dawa na kula chakula na kufanya yote ninayoambiwa na waganga na familia yangu yote nananifanya niendelee kuishi; ili tu mama asije akanizika na baada ya hapo afe kwa uchungu wa kumzika mwanae mpenzi.
Kwa vijana ambao hawajapata maambukizi ya VVU jikingeni, jikingeni hata
kama siyo kwa faida yenu lakini kwa faida ya wazazi wenu. Inauma sana
mzazi anapomzika mwanae kwa uchungu. Kawaida siyo wazazi kuzika watoto
ila kwa watoto kuzika wazazi.
Tuandikie taarifa fupi jinsi unavyoteseka na UKIMWI. kupitia kiboksi cha kutuma maoni kilichopo pembeni kulia au tuma kupitia e-mail; afyatele@gmail.com Tutachapisha bila jina au simu namba yako kama hutotaka vitokee hapa
2. Stori ya Skolastika
Mimi naitwa Scolastica.
Mwaka jana nilikuwa naumwa umwa kila mara. Nakohoa, nina homa, natoka
jasho na ngozi yangu ina vipele pele. Mwezi Septemba 2011 niliamua
kwenda kupima nikaambiwa nimeishaambukizwa na VVU. Nililia
sana. Niliwafikiria wanangu. Nilijua kuwa nilikuwa nafa. Nitakufa na
nitawaacha wanangu wakiteseka humu ulimwenguni. Baada ya ushauri nasaha
nilijisikia afadhali, nilizoea na kuendelea kupigana na ugonjwa wangu.
CD4 zilikuwa zimepungua sana kwa hiyo nikaambiwa nianze dawa za
kurefusha maisha mara moja. Tangu nianze kutumia dawa za kurefusha
maisha najisikia vizuri. Afya yangu ni nzuri; siumwi umwi tena, nakula
vizuri, nafanya mazoezi na nimenenepa kidogo.
Kuambukizwa na VVU siyo
kwamba Mungu hakupendi. Wewe siyo mtu mwovu kuliko wengine. Ni kwamba tu
umeambukizwa na kwa sasa ni lazima upigane na ugonjwa wako na siyo
kusikitika maana kusikitika hakutawaondoa hao VVU mwilini mwako. Huu ni
ugonjwa. Ulimwenguni humu kuna magonjwa mengi. Huu ni mojawapo ya
magonjwa mabaya na ukiwa nao ujue tu wewe hupo peke yako. Kuna wenzako
mamilioni ambao wanateseka kama wewe.
Ukipata VVU siyo kwamba umejamiana ovyo ovyo tu. Kuna ambao wanapata
hata bila kujamiana, kuna ambao wanaupata bila hata kutembea nje ya
ndoa. Unaweza kupata maambukizi kwa njia nyingi.
Nilimwambia mwajiri wangu
kuwa nilikuwa na VVU. Bosi wangu ni mwanamke kama mimi. Alinionea
huruma akanipa msaada na nikaendelea kufanya kazi.
Kuwaarifu watu kuwa unaumwa ni jambo zuri lakini chagua wale ambao unaona watakupokea, watakuonea huruma na hawatakutenga. Kama baada ya watu kujua una VVU; wakianza kukutenga, kukunyanyapaa, achana nao. Waache waishi maisha yako na wewe uishi maisha yako.
Mkakati wako ni, “Mpende akupendaye; asiyekupenda; achana naye”
Kuwaarifu watu kuwa unaumwa ni jambo zuri lakini chagua wale ambao unaona watakupokea, watakuonea huruma na hawatakutenga. Kama baada ya watu kujua una VVU; wakianza kukutenga, kukunyanyapaa, achana nao. Waache waishi maisha yako na wewe uishi maisha yako.
Mkakati wako ni, “Mpende akupendaye; asiyekupenda; achana naye”
Sasa najiangalia na
kuishi maisha yangu siku kwa siku nikimwomba Mungu. Kila ninapoanza siku
mpya; kila ninapoamka asubuhi naanza kwa kusali na kumshukuru
Mungu kuwa nimeona siku mpya kwa kuwa najua usiku uliopita wengi
wanaougua ugonjwa wangu hawakuona siku hii. Ikifika jioni ninapoingia
kitandani kulala namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunilinda siku nzima na
kunifikisha usiku wa leo.
Najua wengi walio na ugonjwa huu hawakuiona
jioni ya leo. Kuna wengi wanaoumwa ugonjwa wangu na
wamekufa asubuhi hii, mchana au jioni hii. Naweka roho yangu mikononi
mwa Mungu na kumwomba kama ataamua aniamshe asubuhi, lakini kama
sikuamka anipokee kwake baada ya mateso haya hapa ulimwenguni.
Wakati ujao tutasoma stori ya Aisha ambaye mpenzi wake anayesoma chuo kikuu, inavyoonekana amemwambukiza VVU
Msomaji tuandikie stori
yako kama na wewe umeishawahi kuambukizwa au unamjua mtu aliyeambukizwa
awe ndugu, rafiki, mfanyakazi mwenzako au jirani. Wataalamu tuandikieni
mnavyomwona huyu mama na mnavyoona ugonjwa huu wa hatari: tuandikie kupitia kiboksi cha maoni kilichopo pembeni kulia au tuma kupitia e-mail; afyatele@gamil.com (kila utakachotuma kwa kupitia kiboksi cha maoni au e-mail, itakuwa ni siri, mpaka utakaporuhusu kuposti hewani)
0 comments:
Post a Comment