Ukatili wa kijinsia au UWAKI ni ukiukwaji wa haki za binadamu ambapo mtu kwa kutumia maungo, hisia za kujamiana au kujamiana, au hisia za akili na kisaikolojia anamsababishia madhara mtu mwingine kwa kuwa yeye yeye mtuhumiwa anayesababisha madhara, anajisikia au anaamini kuwa ana uwezo na mamlaka juu ya mwathirika yaani huyo anayemthuru.
UWAKI hujumuisha vitendo anavyofanyiwa mwanamke au mwanamme (mwathirika)
bila ridhaa yake kutokana na mwanamme au mwanamke anayevifanya
(mhalifu) kufikiria kuwa ana madaraka dhidi ya mwathirika.
Ukatili
wa Kijinsia ni pamoja na kujamiana bila ridhaa ya mwathirika kihisia na
kwa kutumia viungo vya siri, ukatili wa kimwili na wa kisaikojia,
kufanya vitendo vya jadi vyenye madhara kama kukekeketa wasichana na
wanawake na ukatili wa kiuchumi na wa kijamii.
Ukatili huu unawalenga watu kwa misingi ya kijinsia kwamba wao ni wanawake au ni wanaume basi wanafanyiwa vitendo hivyo.

Ukatili wa Kijinsia
ni ukatili unaotokea kati ya wanaume na wanawake ambapo kawaida
anayefanyiwa ukatili ni mwanamke. Ukatili huu unatokana na kutokuwa na
uwiano wa mamlaka walio nao watu wa jinsia ya kike na ya kiume, wanaume
wakionekana au wakifikiri kuwa wana mamlaka zaidi dhidi ya wanawake na
hata wanawake nao wakifikiri kuwa wanaume wana mamlaka zaidi kuliko wao.
Wanawake
ndio hasa wanaofanyiwa ukatili kwa kuwa tu ni wanawake kwa hiyo pamoja
na kuwa ukatili wa kijinsia unahusisha jinsia zote mbili, akina mama
ndio hasa wanaoadhirika zaidi. Ukatili wa kijinsia ni pamoja na kutumia maungo, ukatili unaohusu kujamiana na unaohusu kuathirika kiakili.
Akina
mama wengi na akina baba wachache wanateseka sana kimya kimya katika
ndoa au mahusiano kutokana na kufanyiwa vitendo vya UWAKI. Aina za
ukatili wa kijinsia ni kufanya ukatili kutumia maungo, ukatili unaohusu
kujamiana, unaohusu mateso ya kiakili, unaotokea kwenye familia, ukatili
kwa watoto, ubakaji, ubakaji
unaotokea kwenye mahusiano ya ndoa, unyanyasaji wa kijinsia pahala pa
kazi, mashuleni na kwenye vyuo; kuingizwa kwenye shughuli za umalaya kwa
nguvu, kusafirishwa kwenda kufanyishwa kazi au umalaya na kukeketwa kwa wasichana na akina mama.
Ijapokuwa
tunasema kuwa akina mama na wasichana ndio hasa wanaofanyiwa ukatili wa
kijinsia ukweli ni kuwa hata wanaume na vijana wa kiume wanafanyiwa
ukatili wa kijinsia....
Taarifa
juu ya unyanyasaji dhidi ya wanawake na wasichana, ikiwa ni pamoja na
unyanyasaji wa majumbani, ubakaji ndani ya ndoa na ndoa za wasichana
wadogo, bado ni tatizo kubwa hapa Tanzania. Ukeketaji wa wasichana unaendelea kama kazi yaani ni mazoea, ikiwa ni pamoja na hata kwenye baadhi ya maeneo ya mijini.
Kuna ripoti na mashtaka machache sana ya waathirika wa Ukatili wa Kijinsia (UWAKI) wakiwashtaki
waliowafanyia ukatili. Kati ya kesi hizi ni chache sana zinafika
mahakamani na hata zile zinazofika mahakamani ni chache sana zinafikia
kutolewa hukumu
WashikajiWakijadiliana:
Mshikaji 1: Jana jirani yangu alitusumbua sana
kwa makelele usiku. Mwanamme alikuwa analia kwa nguvu “Ntakuua!
Ntakunyonga! ntakumaliza!” na huko tunasikia mangumi Pa! Pa! Pa! Pa!
Mshikaji 2: Ndio ilivyo; sisi akina baba wakati mwingine ni wakatili. Tunawadunda sana wake zetu. Siku moja nao watatudunda.
Mshikaji 1: Kwani
aliyekuwa anadundwa ni mke basi. Tulipokimbilia nyumbani kwao tulimkuta
mke amemwangusha mme wake na amemkalia tumboni; anamdunda sawa sawa.
Kumbe mwanamme kwa kulia kule alikuwa anaomba msaada lakini hakutaka majirani tujue kuwa aliyekuwa anadundwa ni yeye mwanamme.
Ameneh Bahrami sasa ni kipofu
Huko Iran mwaka wa 2004 baba mmoja
alimwagia tindi kali dada mmoja kwa kuwa eti alikataa awe mchumba wake;
alimkatalia penzi kwa hiyo akamwagia tindikali machoni na kumsababishia
majeraha usoni na upofu.
Huu ndio ukatili kweli kweli. Ni UWAKI
kwa kuwa huyu baba kafanya hivyo kwa kuwa ana hisia kuwa eti kwa kuwa
ni mwanamme basi ana pawa (power) kuliko wanawake na mwanamke hawezi
akamkatalia penzi. Kwa kuwa yeye ni mwanamme basi akimtongoza mwanamke
basi ni lazima huyo mwanamke amkubalie.
Baada
ya kumwagia tindikali na kumsabaishia makovu usoni na upofu, mahakama
ya huko Irani iliamua kuwa kwa kuwa sheria za nchi hiyo zina misingi ya jino kwa jino
basi huyu baba amwagiliwe naye tindi kali usoni kwenye macho naye
apofuke. Waliamuru kuwa aende hospitali na huyu mama akishirikiana na
daktari wamwekee tindi kali machoni. Adhabu hiyo ilikuwa itekelezwe mwezi wa saba mwaka
wa 2011. Baba alipelekwa hospitalini na daktari akajiweka tayari
kumdondoshea matone ya tindi kali kwenye macho. Mara akafika yule mama
na kusema kuwa anamsamehe!
Mama
huyu mwenye huruma alikuwa amesindikizwa hospitalini humo na ndugu zake
wawili wakimshikia kulia na kushoto. Akionekana na makovu yake usoni na
machoni na kwenye mdomo; alionekana kuwa ni mama mwenye maumivu makubwa
rohoni lakini alikuwa na moyo wa huruma. Alimsamehe mbaya wake
aliyemsababishia vilema vya maisha usoni na upofu.
Mama
huyu anayeitwa Ameneh Bahrami alisema, “Ni vema mtu usamehe, sitaki
kulipiza kisasi.’ Mbaya wake Majid Movahedi alipiga magoti na kushukuru
akilia huko akiushikilia ukuta.
Sheria
ya jino kwa jino inayojulikana kwa jina la ‘qisas’ (kisas) inasema kuwa
pale mtu ameleta majanga basi familia yake au yeye mwenyewe huomba
radhi; humwomba aliyedhurika
asamehe na kukubaliana fidia bila hivyo sheria ya jino kwa jino ichukue
mkondo wake. Kwa hali hiyo mwaka wa 2010 jamaa mmoja ilibidi akatwe
mkono wake kwa kuwa alitenda kosa ambalo aliyemtendea hakukubali
asamehewe.
Huyu
mama ambaye sasa ana vilema vya maisha, baada ya msamaha huo; huyu baba
itabidi akae gerezani mpaka mahakama itakapoamua apewe adhabu gani
nyingine ambayo ni pamoja na kumfidia huyu mama aliyekuwa kipofu na uso
wake kuharibika.
Shirika la Haki za Binadamu (Amnesty International)
wanaipinga sheria hii ya Iran ambayo inampa mtu adhabu ya kutegemea na
kosa alilofanya. Kama amemfanya mtu kipofu basi naye apofuliwe. Kama
amemkata mtu mkono naye akatwe mkono. Kama ameua naye auawe. Kama jicho
likiharibiwa kwa kuwa alimwagia huyu mama tindi kali, basi na yeye
amwagiliwe tindi kali machoni asikie maumivu makali kama
aliyomsababishia aliyemjeruhi. Shirika
la ‘Amnesty International’ linasema eti pamoja na kwamba mtu amefanya
kitendo cha ukatili siyo vizuri naye kumfanyia mbaya wake ukatili.
Kitendo cha kinyama kikifanyika na kumjeruhi mtu ni kwamba
kimeishafanyika. Kumfanyia unyama aliyekifanya hicho kitendo inakuwa ni
unyama mkubwa zaidi. Siyo sawa kumfania vibaya mtu aliyefanya ubaya eti
kwa kulipiza kisasi!
Msomaji hili linakuingia kichwani? na wewe unasemaje na hili? tuandikie mawazo yako na uzoefu wako juu ya unyanyasaji wa kijinsia.
Wewe mwenyewe au jirani au ndugu yako amenyanyaswa au kufanyiwa ukatili
wa kijinsia? tuandikie kupitia kiboksi cha maoni kilichopo pembeni kulia au tuma kupitia e-mail afyatele@gmail.com
0 comments:
Post a Comment