UNYONYESHAJI wa maziwa ya mama kikamilifu umeelezwa na wataalamu unasaidia mama asipate ujauzito mwingine mapema.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk Salim Robert alisema hiyo ni njia mojawapo ya kupanga uzazi na hivyo humpa mama muda wa kupumzika na mwili wake kujijenga upya.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk Salim Robert alisema hiyo ni njia mojawapo ya kupanga uzazi na hivyo humpa mama muda wa kupumzika na mwili wake kujijenga upya.
Aidha kwa upande wa mtoto, Dk Robert alisema maziwa hayo yana faida nyingi ikiwemo kumpatia virutubisho vyote anavyohitaji kwa uwiano sahihi kwa afya na ustawi.
Yana viini vya kingamwili vinavyofanya kazi kama chanjo dhidi ya maradhi na humeng’enywa na kufyonzwa kirahisi zaidi mwilini tofauti na vyakula vingine.
Alisema mtoto anatakiwa kunyonyeshwa maziwa ya mama pekee katika kipindi cha miezi sita baada ya kujifungua na baada ya hapo, inaruhusiwa kumpa vyakula vingine huku akiendelea kunyonya mpaka afike miezi 24.
Alisema hayo wakati Mkoa wa Iringa ukiadhimisha kitaifa wiki ya unyonyeshaji duniani iliyofanyika mjini Mafinga, wilayani Mufindi kati ya Agosti Mosi na 7, mwaka huu.
Akizungumzia sababu za kuwepo kwa maadhimisho hayo, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk Christine Ishengoma alisema inatokana na mmomonyoko wa kimaadili ambao moja ya madhara yake ni kupunguza kasi ya unyonyeshaji watoto maziwa ya mama.
Dk Ishengoma alisema hivi sasa watoto wamekuwa wakipewa maziwa mbadala ya kopo na kuingizwa katika matumizi ya chupa na nyonyo bandia za kulishia watoto.
Alisema matumizi hayo yameongeza kasi ya biashara ya maziwa maalumu ya kulisha watoto wachanga na wadogo pamoja na bidhaa zinazoambatana na maziwa hayo kuongezeka huku zikilenga wanawake ambao hawahitaji maziwa hayo.
Alisema ulishaji mbadala kwa watoto huchangia katika ongezeko la maradhi ya kuhara, mfumo wa kupumua na tatizo la watoto kuwa na uzito uliozidi na kiribatumbo.
Kwa mujibu wa takwimu, ni asilimia 49 pekee ya wanaojifungua wanaowaanzishia watoto wao kunyonya maziwa ya mama katika muda sahihi.
“Takribani asilimia 30 ya watoto wachanga hupewa maji, vinywaji au vyakula kabla hawajaanza kunyonyeshwa,” alisema.
KWA HISANI YA HABAILEO
0 comments:
Post a Comment