Mirija hii ndiyo inayosaidia kushusha yai kutoka kwenye kokwa na kupandisha mbegu ili vikutane humo ndani ya mirija na kuumba binadamu.
Tulisema kuwa mirija hii ikiziba baada ya kutoa mimba basi huyu mama au msichana hatapata mimba tena.
Haya ndiyo yaliyomtokea msichana mmoja aliyejitambulisha kwa jina moja la Jasinta baada ya kutoa mimba kama anavyotuhadhithia katika stori hii ya kweli na ya kusikitisha.
Jasinta anajuta kutoa kwake mimba alipokuwa msichana mdogo wa umri wa miaka 18. Anasema hakujua utoaji mimba unaweza ukawa na matatizo mengi kama aliyo nayo sasa.
Alipokuwa sekondari alikuwa na rafiki yake wa kiume na mara akapata mimba. Rafiki yake kusikia ana mimba alimwambia kuwa hana habari naye tena na baada ya muda hakuonekana tena.
Alijisikia vibaya kuwa ataishije na hiyo mimba, kuilea na kuzaa na kumtunza mtoto. Ilikuwa ni mimba yenye matatizo, shida na tabu kama zile 12 nilizokusimulia na ukazisoma miezi miwili iliopita.
Jasinta aliishi na wazazi wake na hakuthubutu kuwaambia hata kumwambia mama yake kwamba ana mimba. Hakukuwa na kliniki ambapo angeweza kwenda na kujieleza kuwa ana mimba na kupata ushauri juu ya mimba hiyo.
Alimweleza shangazi yake na kumwambia kuwa alitaka kuitoa hiyo mimba. Shangazi alimwambia kuwa kuna hospitali moja anayoifahamu iliyokuwa inatoa mimba.
Kwani mwanawe alikuwa na mimba na akaenda kuitoa hapo.
Jasinta anahadithia kwa uchungu yaliyompata.
‘Nilienda hapo asubuhi nikiwa na rafiki yangu. Rafiki yangu hakuruhusiwa kukaa na mimi wakati wa ‘procedure,’ yenyewe kwa hiyo aliona ni heri arudi nyumbani na kunifuata baadaye.
“ Nilikuwa peke yangu na waganga (madaktari) wawili wa kiume. Palikuwa pasafi, kila kitu kikionekana kama kina rangi nyeupe.
“Nikawa na matumaini kuwa kila kitu kitakuwa sawa lakini mambo hayakuwa sawa. Waganga walinilaza kitandani wakanipima na kuniambia kuwa nilikuwa na mimba inayokaribia miezi minne.
“Walichukua kidonge cheupe cha kuua mimba yenyewe, yaani cha kuua mtoto, wakakiingiza kwenye kizazi changu. Niliambiwa nipumzike kitandani.
“Baada ya saa nne niliambiwa nihamie kwenye kitanda cha upasuaji ili mimba itolewe. Nilikuwa mimi na madaktari hao wanaume wawili.
“Walinipiga sindano ya kunifanya nisisikie maumivu lakini wakati wote nilikuwa macho kabisa nikiona na kusikia kila kitu. Yote niliyoona yalitisha.
“Damu, uchafu uchafu, vipande vipande vya mwili wangu na vya mwili wa mtoto wangu vikiwa na damu kila pahala, ilikuwa ni hali ya kutisha.
“Kama ningejua kuwa ‘procedure,’ yenyewe ya kutoa mimba ni yenye maumivu na matatizo kiasi hicho ni heri tu ningeiacha mimba yangu ikue, nizae na kulea mtoto.
“Baada ya muda nikaanza kusikia maumivu. Wakaniambia nivumilie maana ilikuwa lazima kuharakisha na kumaliza shughuli yenyewe.
“ Baada ya kumaliza maumivu yalizidi, nafikiri ni ile dawa ya ganzi iliisha, walinipa kidonge cha Panadol nikaendelea kuumwa huku damu ikinitoka.
“Wakati wote nilifikiria kuwa hospitali hii haikuwa inanipa huduma nzuri. Kwa nini hawakunipa dawa ya kutosha kuua, kumaliza au kupunguza maumivu? Walinirudisha kitandani nipumzike.
“Saa 12 jioni nilipopewa ruhusa mwenzangu alinifuata lakini waliponiruhusu kwenda nyumbani niliwaambia bado damu inatoka.
“Wakaniambia nisiwe na shaka, itaisha baadaye. Baada ya siku mbili bado damu ilikuwa inatoka nyingi na nilikuwa naumwa tumboni sana. Nilikuwa najisikia kama nina homa, nilirudi hospitalini pale wakanifanyia CT scan.
“Waliona bado kulikuwa na vitu yilivyobakia ndani ya kizazi changu. Wakaanza tena upya kutoa vilivyobakia ndani. Walinilaza kitandani na kunipa sindano ya kupunguza maumivu.
“Nikiwa macho kabisa wakaendelea kutoa yaliyobaki humo ndani. Nakwambia niliumwa, niliumwa sana. Maumivu yalikuwa makubwa kuliko ya siku ile ya mwanzo. Niliwasikia wakiambiana kuwa sihitaji kuongezewa damu.
“Ukweli kama nilihitaji huduma ya kuongezewa damu ingebidi wazazi wangu waambiwe nimetoa mimba na nahitaji kuongezewa damu. Aibu! Aibu! kwenye familia. Sijui ningeweka uso wangu wapi hapo nyumbani kwa baba yangu.
Matatizo ya utoaji mimba niliofanya nikiwa na umri wa miaka 18 sasa yamenifuata nikiwa na umri wa miaka 28. Sasa nimeolewa na kwa muda wa miaka miwili natafuta mtoto. Wenzangu nilioolewa nao tayari wameishabeba mimba na wengine wamekwisha kuzaa wakati mimi bado nahangaika,” anasema.
“Nilienda Hospitali ya Marrie Stopes...nilikuwa na wasi wasi labda wale waganga wakati ule nilipotoa mimba walinitoa kizazi changu.
“Huko Marrie Stoppes wamenipima vizuri sana na kuona bado kizazi changu kipo. Lakini basi, mirija ya kizazi imeziba. Imeziba kwa sababu ya ile shughuli niliyofanya miaka 10 iliyopita.
Anasema daktari wa Marrie Stoppes alimuuliza kama ameshawahi kutoa mimba na alipomjibu ukweli alionekana kama anatingisha kichwa chake, akasema, “Kumbe ndiyo sababu mirija imeziba.”
“Siwezi nikapata mimba tena. Hakuna habari ya mimba tena kwangu. Ile mimba niliyotoa ilikuwa ni mimba yangu ya kwanza na ya mwisho. Ningejua kuwa kuna uwezekano wa kutopata mimba tena nigeiacha ile mimba tu wakati ule.
“Ningeilea kwa njia yoyote tu. Niliitoa na sasa sipati nyingine tena. Mtoto aliyeuawa na kutolewa kwenye mimba ile angekuwa na miaka 10 sasa. Sijui hata alikuwa wa jinsia gain, sijui wa kiume au wa kike.
Anasema hawezi kupata mtoto na hajui ndoa yake itakuwaje bila mtoto. Hajui mume wake atajisikiaje akijua kuwa hataitwa baba watoto na yeye haitatokea aitwe mama watoto.
Jasinta anaendelea kusema: “Kinachonifanya kujisikia vibaya ni kwamba sikuweza kupata habari popote juu ya utoaji wa mimba kuwa inatolewaje na kuna matatizo gani yanayoweza kutokea.
“Ningejua kunaweza kutokea matatizo haya na yale ningeweza kufikiria vizuri na kuamua kutoitoa,” anasema.
Jasinta anasikitika kuwa alikwenda kutoa mimba bila kujua kuwa wanafanya nini katika shughuli hiyo na utoaji mimba una madhara gani.
Baada ya kujua kuwa utoaji mimba unaambatana na matatizo makubwa kama yale tuliyoandika kwenye makala mbili zilizopita na hili kubwa alilotuhadithia Jasinta, inabidi tuseme kuwa utoaji mimba ni kitu ambacho kisingepaswa kufikiriwa kabisa katika kutatua tatizo la mimba ambayo haikutarajiwa.
Wengine wanasema ni kitu ambacho hakipo kwenye listi mojawapo ya vitu vya kufanya kama mimba haikuwa kwenye mpango,” kwani madhara yanayotokea ni makubwa mno.
Acha mimba ikue, uzae utakuja kuona baadaye faida uliyopata kwa kuicha ikue na kuzaa. Ukiitoa kama hutapata matatizo ya kifo baadaye utakuja kuona hasara zinazotokana na kutoa hiyo mimba.
Wanawake wengi wanaona kutoa mimba kama ni jambo la kawaida sana. Huenda kwenye vihospitali vya mitaani wanapotoa mimba na kujipatia huduma hiyo bila kujua matatizo yanayoweza kutokea wakati wa kutoa na baada ya kutoa mimba.
Wengine huenda kwenye hospitali nzuri tu kama alivyoenda Jasinta lakini ukweli ni kwamba hata kwenye hospitali kubwa na nzuri kuna hatari wakati wowote kupata matatizo wakati wa kutoa mimba na baada ya kutoa mimba.
Utoaji mimba kwa kweli si vizuri. Ni ‘procedure,’ yenye matatizo mengi. Ni heri uiache mimba yenyewe ikue na uzae hata kama umeipata bila kukusudia.
Kwa hisani ya Threewhite
0 comments:
Post a Comment