AMA kweli
hujafa hujaumbika, mrembo Khadija Omar, mkazi wa Kigogo, Dar amepata
pigo kufuatia kupofuka macho alipokuwa akiwekwa nyusi bandia katika
saluni moja iliyopo maeneo hayo, Risasi Jumamosi lina mkasa mzima. Tukio hilo lilitokea Novemba 14, 2013 na kuvuta hisia za watu wengi waliosikia na kushuhudia mkasa huo.
Akizungumza
na paparazi wetu juzi huku akimwaga machozi, Khadija alisema siku ya
tukio saa 11 jioni alikwenda kwenye saluni hiyo iliyopo jirani na
anapoishi kwa lengo la kubadili mwonekano wake wa macho kama akina dada
wengine wanavyofanya.
“Mara tu baada
ya kunibandika kope nilianza kuona giza, nikawaeleza akina dada
waliniweka lakini wakanipuuza na kuniambia mimi ni mwoga.
“Muda mfupi
mbele hali yangu ikawa mbaya zaidi, ikabidi wazibandue kope lakini
juhudi zao ziligonga mwamba kwa sababu walitumia gundi kali, ikabidi
nirudi nyumbani,”alisema Khadija.
Akaongeza:
“Nikiwa njiani macho yaliniuma sana na kuzidi kupoteza uwezo wake wa
kuona, ghafla nikaanguka chini. Akatokea msamaria mwema na kunipeleka
nyumbani,” aliongeza.
Khadija alisema
kesho yake alikimbizwa Hospitali ya Amana, Dar ambako alipatiwa dawa
bila ya kutolewa kope hizo na kuruhusiwa kurudi nyumbani.
“Nilipofika
nyumbani hali ilizidi kuwa mbaya nikalazimika kupelekwa Hospitali ya
Macho ya CCBRT (Msasani, Dar) ili kupatiwa ufumbuzi wa tatizo hilo,”
aliongeza Khadija kwa majonzi.
Alisema kule CCBRT alijikuta akiangua kilio baada ya madaktari kumwambia kope hizo haziwezi kutolewa mpaka zikatwe na mkasi.
Baada ya zoezi
hilo kufanyika, Jumapili iliyopita Khadija aliweza kufungua macho kwa
mara ya kwanza tangu alipotokewa na hali hiyo lakini bila kuona
sawasawa.
Jumatatu
iliyopita Khadija aliruhusiwa kurudi kwake lakini akiwa hana uwezo wa
kuona na kutakiwa kurejea tena hospitalini hapo baada ya wiki tatu kwa
uchunguzi zaidi.
Daktari mmoja
wa CCBRT ambaye hakuwa tayari kutaja jina lake gazetini alisema:
“Khadija anaweza kuona kama zamani lakini itamchukua muda mrefu kutokana
na madhara ya gundi ya ‘supa glu’ iliyotumika.
Taarifa zaidi
zinasema, Jane na Koku wafanyakazi wa saluni waliomuweka kope hizo
Khadija walikamatwa na Polisi wa Kituo cha Magomeni jijini Dar na
kufunguliwa jalada la uchunguzi namba MGN/RB/13021/2013.
Kwa hisani ya GPL
0 comments:
Post a Comment