
Wakati
anasumbuka na masuala ya viza, alihisi kuwa na hali isiyokuwa ya
kawaida, aliamua kununua kipimo cha ujauzito cha bei nafuu.
Kwa bahati mbaya aligundua kuwa alikuwa mjamzito ambao anahisi kuupata siku alipobakwa na Wanigeria wanne.
Munira
anasema suala la yeye kushika ujauzito lilileta shida zaidi, kwani
mwenyeji wake, Jacky alimweka kikao na kumsuta kwa hilo bila kujali kuwa
alibakwa. Mmoja wa wanawake hao ambao walikuwa wakifahamika kama ‘Boss
Lady’ alimshauri kuwa atamtafutia mwanaume ambaye atamsaidia kutafuta
daktari ili watoe mimba hiyo.
Alipofika
kwa daktari, alipewa vidonge tisa ambavyo alitakiwa kulipia Yuan za
China 600 (zaidi ya Sh100,000). Hakuwa na fedha hivyo alitakiwa
kuendelea kujiuza licha ya kuwa hakuwa amepona ili apate fedha hizo.
“Baada ya
muda nilipata fedha hizo na nilipewa vidonge, ambavyo hata hivyo
haviharibu mimba kwa wakati huohuo bali taratibu sana,” anasema Munira.
Muda wa
kuishi Guangzhou ulikuwa umekwisha na Munira hakuwa amepata viza,
ilimbidi aondoke. Lakini mwenyeji wake alimwambia ni lazima atafute
fedha ya kulipia viza usiku uleule. Akimaanisha akajiuze usiku huo na
kupata fedha kwa ajili hiyo.
Munira
alilazimika kuingia mitaani usiku ule kusaka wateja kwa ajili ya kupata
fedha za kwenda kuchukua viza hiyo Macau, jimbo jingine maarufu nchini
China.
Mwenyeji wake alimwambia wakati anaondoka asubuhi siku inayofuata, asiondoke bila kumuaga.
Aliporejea usiku wa manane alijiandaa kwa ajili ya safari ya asubuhi yake, licha ya kwamba hakuwa amepata fedha za kutosha.
Kulipopambazuka
alikwenda kumuaga mwenyeji wake kama alivyoambiwa, lakini alishangazwa
na kitendo cha mwenyeji huyo kumnyang’anya baadhi ya vitu kama nguo na
viatu alivyomnunulia wakati alipofika nchini humo.
Wakati
akiondoka alisindikizwa na Mtanzania, msamaria mwema, ambaye alimpa Dola
400 za Marekani kama akiba na nauli ya Yuan 50, hivyo kuongezea katika
fedha alizokuwa amepata usiku ule.
Macau ni ‘Boda la JK’
Munira
alichukua treni ya kuelekea Macau, mpakani lakini aliambiwa akiwa huko
anatakiwa atoke kwa saa 12 kila baada ya miezi mitatu ili atakaporudi,
aanze kuhesabiwa tena siku za kuishi.
Macau ni
jimbo ambalo Watanzania wanapata msamaha wa kukaa kwa siku 90 bila viza,
hivyo mara nyingi siku zinapokaribia kuisha, Watanzania katika jimbo
hilo huondoka kwa saa 12, kisha kurejea kama wageni ambao huanza
kuhesabiwa siku zao upya.
Kutokana na
urahisi huo wa kimaisha, Macau umebatizwa jina na Watanzania ambao
wanauita ‘Boda la Kikwete’, wakimaanisha kwamba maisha yao katika jimbo
hilo ni kwa hisani ya makubaliano baina ya uongozi wa Rais Jakaya
Kikwete na Serikali ya China.
Wakiwa
Macau, Watanzania huenda kuchukua viza nchi jirani ya Malaysia, kinyume
na hapo hubaki Macau, wakisubiri majaliwa ya kupata viza au kurudi
nyumbani.
“Nilipofika
Macau nilipata shida, Wachina hawajui Kiingereza, nazunguka na begi
langu, kumbuka bado sijapona baada ya kufanyiwa ule unyama,” anasema.
Anasema
alifanikiwa kuvuka mpaka wa Macau kutoka Guangzhou, ingawa alipata shida
kupita katika viunzi vya uhamiaji kutokana na sheria za China.
Akiwa hoi
kwa kuchoka, alikutana na raia wa Somalia ambaye alimsaidia kujaza fomu,
lakini hata hivyo hakuweza kumsubiri, hivyo Munira alibaki peke yake.
“Nilipofika
katika kiunzi cha mwisho cha uhamiaji, nilihojiwa sana, maofisa uhamiaji
walidai kuwa sura yangu ya sasa haifanani na iliyopo kwenye hati ya
kusafiria, hivyo wakawa na wasiwasi na mimi,” anasema.
Munira
anasema maofisa hao walimuuliza maswali mengi kama namba ya pasipoti,
umri, majina matatu, mambo ambayo aliyajibu kwa ufasaha, lakini bado
hawakuridhika na wakampeleka kwenye chumba maalumu cha polisi kwa
mahojiano.
Huko, walimwambia afumue nywele alizokuwa amesukia na kumhoji kwa zaidi ya saa moja kabla ya kumruhusu.
Anasema ni kweli sura yake halisi ilikuwa imebadilika baada ya kukonda sana, kutokana na mateso aliyokuwa anayapata.
“Mwisho wa
siku waliniachia, nikachukue teksi, lakini ilinipoteza. Bahati nzuri
mbele kabisa nikakutana na msichana raia wa Urusi, alichukua namba yangu
na akanielekeza sehemu niliyotakiwa kwenda, huo ukawa mwanzo wa urafiki
wetu,” anasema.
Mjini Macau
Anasema
alipofika eneo aliloelekezwa, katika hoteli kubwa iitwayo St Marol,
aliwakuta wasichana wengi zaidi ya 200 wa Kitanzania ambao viza zao
zilikuwa zimeisha muda.
Walikuwa ni wengi na wote walikuwa wanajiuza.
“Mji huo ni
kama Zanzibar hivi. Ni pazuri na ni mji wa gharama sana kila kitu ni
gharama, hata hivyo wateja hawakuwa wengi kama Guangzhou,” anasema.
Katika hoteli hiyo ya St Marol, wasichana 15 hadi 20 katika eneo hilo, huchangia gharama za chumba.
Alishuhudia
wasichana wadogo kuliko yeye, ambao walimlalamikia wakidai kuwa nao
wanaishi maisha ya kujiuza ili wapate fedha kinachowakwamisha ni kukosa
fedha za nauli ya kuwarudisha nchini.
Munira
aliamua kuwasaidia, hivyo alishauriana na mmoja wao aitwaye Candy kwamba
warekodi sauti kwenye simu wakieleza adha wanazopata, kisha wazitume
Tanzania kupitia WhatsApp ili wapate msaada wa kurudi nyumbani.
Anasema
ujumbe ule wa sauti ulisambaa karibu kwa Watanzania wote wanaoishi
Macau, China, Guangzhou na Hong Kong na kwamba wezao wa Macau waligundua
kwamba sauti hiyo ni ya mmoja wa wasichana wanaoishi kwenye hoteli hiyo
ndipo walipoamua kwenda kuwasuta Munira na Candy chumbani kwako.
“Kundi la
wasichana wa Kitanzania zaidi ya 100 walifika kwenye chumba chetu,
wakaanza kutusuta kwa nini tuliamua kutuma ujumbe wa sauti kama ule.”
“Walitaka
kunipiga wakidai kuwa nawaharibia maisha yao kwani wanapata pesa za
kujenga nyumba na kununua magari kwa kazi hiyo,” anasema.
Anasema yeye
na Candy walipoona hali imekuwa mbaya, waliamua kukimbia. Munira kwa
hofu, alibahatika kubeba hati ya kusafiria, tiketi na kadi ya manjano,
akiacha nguo na baadhi ya mali zake.
Hata hivyo, walipofika njiani, Candy alibadili uamuzi na kuamua kurudi hotelini.
“Nilimshukuru
Mungu kwa kunipa akili ya kuchukua vitu vitatu muhimu, nikampigia simu
rafiki yangu Mrusi, ambaye alikuja kunisaidia na kunipeleka kuishi
kwake.
….Itaendelea
0 comments:
Post a Comment