TUMEZOEA kuanza siku kwa kunywa vinywaji moto kama vile
kahawa au chai na hii imekuwa ndiyo desturi ya maisha ya watu wengi
duniani.
Lakini siyo lazima kuanza siku yako kwa kunywa vinywaji hivyo,
ambavyo tafiti nyingi zimeonesha chai na kahawa vikitumiwa kupita kiasi
vinaweza kuwa na athari kwa mtumiaji.
Katika kuangalia njia
mbadala na bora ya kufungua kinywa na kuanza siku vizuri, imebainika
kuwa glasi moja ya maji ya uvuguvugu yaliyochanganywa na juisi ya limau
kipande kimoja, yana faida kubwa mwilini na yanafaa kutumiwa kama
kifungua kinywa asubuhi.
Zifuatazo ni baadhi ya faida kubwa za kunywa
maji kwa kuchanganya na juisi ya limau asilia kama zilivyoanishwa na
kuthibitishwa na tafiti mbalimbali za kisayansi:
HUSAIDIA USAGAJI CHAKULA:
Maji ya uvuguvugu husaidia kuuamsha na kuuchangamsha utumbo na maji ya
limau hulainisha na kuondoa sumu yoyote inayoweza kuwa imeganda kwenye
utumbo na kuipeleka kweye njia ya haja kubwa ili kutolewa kama uchafu.
HUONDOA SUMU KWENYE NGOZI NA MWILINI:
Unywaji wa maji ya uvuguvugu yaliyochanganywa na juisi ya limau
husaidia sana kuondoa sumu na uchafu kwenye ngozi kwa njia ya mkojo.
Aidha, kiwango kingi cha Vitamin C kilichomo kwenye juisi ya limau
huondoa takataka zote za kwenye mwili na damu, hivyo kuiacha ngozi yako
safi, laini na nyororo.
HUIMARISHA KINGA YA MWILI: Kama
tulivyoona hapo juu, limau lina kiwango kingi cha Vitamin C ambayo ni
muhimu katika kujenga kinga ya mwili na huzuia magonjwa ya mafua na
kikohozi. Halikadhalika limau lina kiwango kingi cha ‘potasiamu’ ambayo
huamsha ubongo na kudhibiti shinikizo la damu.
HUONDOA ULEVI WA KAHAWA:
Kuna watu wameshazoea kunywa kahawa kila siku na kuwa kama ulevi, kwani
wanapokosa kunywa huwa kama wagonjwa, lakini kwa kunywa maji na limau
hali hiyo ya ‘uteja’ huondoka na kujisikia huru na mchangamfu.
HUSAIDIA KUPUNGUZA UZITO:
Limau pia lina kiwango kingi cha kirutubisho aina ya kamba lishe
(pectin fiber) ambacho ukikila kinakufanya ujisikie kushiba. Hivyo maji
haya ni mazuri sana kwa watu wenye kuhitaji kupunguza uzito au
kuimarisha uzito walionao.
MAMBO YA KUZINGATIA KABLA YA KUANZA
Hakikisha
kiwango cha joto cha maji utakayotumia kiwe cha kati, si ya moto wala
baridi. Maji moto sana siyo mazuri kwasababu yataua virutubisho
vilivyomo kwenye limau na ya baridi sana yanaweza kusumbua tumboni. Pia
yawe maji safi na salama.
Ili kuyalinda meno yako dhidi ya uchachu wa
limau, pendelea kutumia mrija kunyonyea maji hayo. Hakikisha unakamua
juisi yako kutoka kipande cha limau halisi na siyo juisi ya limau
iliyosindikwa kwenye chupa.
Ukiwa na mazoea ya kuanza siku yako kwa
kunywa mchanganyiko huu wa maji na juisi ya limau, afya yako itaimarika,
hutapatwa na magonjwa kirahisi na ngozi yako itakuwa laini na nyororo.
Monday, 13 October 2014
- Blogger Comments
- Facebook Comments
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment