Katika tathmini ya haraka ya wadudu ambao wanaweza wakaeneza maradhi mbalimbali ukiacha nzi, nyuki anaweza kuwa mmojawapo.
Kama ilivyo nzi, nyuki hutua maeneo mbalimbali kutafuta malighafi kwa
ajili ya kutengeneza asali. Katika harakati hizo nyuki hutua maeneo
mengi kuchukua vitu muhimu kwa ajili ya kutengeneza asali.
Ingawa nzi anatembea maeneo machafu, wanasayansi wanasema hata maeneo
ambayo nyuki anatembelea kutafuta vitu kwa masilahi yake, kuna vimelea
vya maradhi mengi ambayo yanaweza kumdhuru yeye na hata binadamu
wanapotumia asali.
Kwa sababu hiyo, wanasayansi wanasema hata nyuki yupo kwenye
mazingira ya kusambaza maradhi ingawa asali yake imekuwa ikitumiwa na
binadamu tangu maelfu ya miaka iliyopita.
Lakini swali likaja, je asali ina vimelea vya magonjwa? Hapo jibu
likawa ni kuchunguza kama inaweza ikawa chanzo cha maradhi pale binadamu
anapoitumia.
Wakiwa maabara wakachunguza asali kwa kina na kubaini kuwa haina aina yoyote ya kimelea hai ambacho ni hatari kwa afya.
Ikabidi wajiulize, kulikoni, wakati wanajua kuwa mazingira ambayo anapita nyuki si salama; yana vijidudu wengi hatari?
Kulikuwa na mawazo kwamba huenda nyuki ana namna yake ya kuchukua
vitu katika maeneo anayopita ili asibebe bakteria, fangasi au virusi
ambao ni hatari kutokana na kuwa ni chanzo cha maradhi.
Walipomchunguza wakaona kuwa nyuki wala hana namna ya ajabu
anayofanya. Waliona anaingia kwenye maua hata yale ambayo yana bakteria
au virusi hatari, akabeba ungaunga na umajimaji ulio na sukari kwenye
maua na kuondoka nao.
Kwa kuchunguza hilo ilionekana haiwezekani kwa namna ambayo nyuki
anachukua mali ghafi zake angeweza kubagua vimelea hatari vya magonjwa.
Waswidi wategua kitendawili
Wanasayansi wa Sweden wiki hii wamekuja na kile walichosema ni
kubaini kile anachofanya nyuki ili asali isiwe na vimelea hatari vya
magonjwa.
Katika ugunduzi wao wanasema unaweza ukasaidia fani ya sayansi ya
afya juu ya namna ya kutengeneza dawa za kukabili maradhi mbalimbali
yanayoenezwa na bakteria.
Kumbuka magonjwa mengi, yanayosumbua binadamu yanatokana na jamii ya
bakteria wanaopatikana katika mazingira mbalimbali yanayomzunguka
binadamu.
Wanasayansi hao wa Chuo Kikuu cha Lund nchini Sweden wamenukuliwa na
Shirika la Utangazaji la BBC wakisema wamebaini kuwa katika tumbo la
nyuki kuna kemikali ambazo zinatumika katika kuua aina yoyote ya
bakteria hatari.
Tena wakasema kemikali hiyo huzalishwa na aina nyingine ya bakteria
ambao hawa hukaa ndani ya tumbo la nyuki na kazi yake hiyo ni kutoa
kemikali za kuua vimelea wowote hatari.
Kemikali inayotolewa na bakteria hai ni aina 13 za asidi zinazofanana na zile zinazopatikana kwenye maziwa.
Aina hizo 13 za asidi wamezielezea kuwa zimetengenezwa kwa kanuni maalumu ambayo inaua aina nyingi za bakteria wa maradhi.
“Tunaweza kutumia kanuni ya ina hiyo kusaidia kutengeneza dawa ambayo
haitamuathiri binadamu bali aina nyingi za bakteria hatari kwa afya ya
binadamu,” anasema Dk Tobias Olofsson, mtaalamu wa Kitengo cha Tiba za
Maradhi yaenezwayo na vimelea wa Chuo Kikuu cha Lund.
Uzuri wa bakteria hao waliopo kwenye tumbo la nyuki, anaeleza, ni
uwezo wao wa kuchunguza aina ya kimelea hatari na kutengeneza sumu
inayofaa kumuua.
Kulingana na maelezo ya Dk Olofsson, bakteria hao ni sawa na kiwanda
cha silaha ambacho kina wafanyakazi mahiri ambao wakiona tu aina ya
adui, wanamtambua na mara moja wanaunda silaha ya itakayotumika
kumuangamiza kulingana na umbile lake na maarifa yake katika kujihami.
“Inaonekana kuwa mtindo huo kwa nyuki umedumu kwa mamilioni ya miaka
na ndiyo maana nyuki hawadhuriki kiafya na asali wanayotengeneza ni
salama pia kwa afya ya binadamu kwa sababu haina vimelea wa maradhi,”
anasema mtaalamu huyo.
Kwa njia hiyo anasema asali ya nyuki huweza kubakia kwa muda ikiwa
hai kwa maana ya kwamba kutoweza kuingiliwa na bakteria hatari kiafya.
Namna asili inavyotengenezwa
Nyuki anaanza kutengeneza kwa kutembelea maua ili kukusanya mali ghafi za kutengeneza asali.
Kwa kawaida nyuki huvutwa na aina fulani ya umajimaji kwenye maua
ijulikanayo kama nectar ambao huvutia wanyama ambao katika kuyavuna
hujikuta wanausaidia kupevusha.
Upevushaji huo unatokana na kusaidia poleni – mbegu za kiume ambazo
zipo katika hali ya unga na kumwagika kwenye ovary – sehemu ya kike ya
ua.
Wakati wa kutengeneza asali, nyuki hutoa vimeng’enyo kadhaa ambavyo
katika hatua tofauti hufanikiwa kugeuza sukari iliyopo kwenye nectar
kuwa sucrose, glukosi na fructose na baadaye ni gluconic ambayo ni
asali.
Wednesday, 29 October 2014
- Blogger Comments
- Facebook Comments
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment