Mazingira ni jambo lingine linaloathiri
afya. Iwapo maji tunayokunjwa na kutumia ni safi na salama, iwapo hewa
tunayovuta si chafu, maeneo tunayofanyia kazi ni salama na pia nyumba
tunazoishi, basi afya zetu huwa salama zaidi ikilinganishwa na watu
wanaoishi kwenye maeneo yasiyo na maji safi na salama au kuvuta hewa
chafu na kufanya kazi kwenye mazingira ya hatari. Uchunguzi uliofanywa
na chuo kikuu cha Zuyd nchini Uholanzi umeonesha kwamba, kuvuta hewa
iliyochafuliwa kwa gesi za magari kwa lisaa limoja kunatosha kumpatia
mtu mfadhaiko wa kifikra au stress katika ubongo wake. Utafiti mwingine
uliofanywa na chuo kikuu cha India cha Purdue umebainisha kuwa, sumu
kali inayotokana na sumu ya risasi, inayoweza kuiingia mwilini mwa
binadamu kutokana na kula vitu vilivyoingiwa na sumu hiyo, nchini
Marekani huathiri maelfu ya watoto kuliko kiwango dhaifu cha sumu hiyo
kinachoweza kuwepo katika vifaa vya kuchezea na mapambo
yanavyosafirishwa.
Afya ya binadamu pia huweza kuathiriwa
na watu wanaomzunguka. Iwapo una familia unayoiangalia au marafiki
katika jamii yako, basi una nafasi kubwa ya kuimarisha afya yako kuliko
mtu ambaye anaishi pekee au hana familia na marafiki. Uchunguzi
uliofanywa na chuo kikuu cha Washington nchini Marekani umegundua kuwa,
ushirikiano wa kifamilia ni jambo zuri kwa mtu na hupunguza kesi za atu
kujiua, hasa wale wanaopatwa na matatizo ya mfadhaiko wa kifikra au
wanapokuwa na fikra ya kutaka kujiua. Vilevile tamaduni, mila na
desturi za jamii na jinsi watu wanavyozithamini itikadi hizo, zina
mafasi kubwa katika afya zao ingawa matokeo yake huweza kuwa mazuri au
mabaya. Kwa mfano mazoea na mila ya kuwakeketa au kuwatahiri watoto wa
kike na wanawake ina madhara makubwa kama vile kuongeza kiwango cha
maambukizo ya magonjwa na hata matatizo ya kiakili miongoni mwa
wasichama na wanawake wanaofanyiwa jambo hilo. Utafiti uliochapishwa
katika Jarida la Afya ya Jamii na Elimu ya Magonjwa ya Mlipuko
umebainisha kuwa, wakati vijana wanapovaa mavazi kwa mujibu wa mila na
tamaduni za makundi au makabila yao, suala hilo huweza kuwapunguzia
uwezekano wa kupatwa na matatizo ya kiakili baadaye maishani.
Urithi wa jenetiki ni suala jingine
linaloathiri afya za watu. Kuishi muda mrefu, siha ya mwili kwa ujumla
na kupatwa na baadhi ya magonjwa na hata kuzaliwa nayo, ni masuala
yanayoainishwa na jinsi jeni zetu zilivyo mwilini tangu wakati
tunapozaliwa. Mambo mengine ni pamoja na vyakula tunavyokula, harakati
zetu kifizikia, tabia na mazoea tofauti kama kuvuta sigara au kunywa
pombe na kutumia madawa ya kulevya. Pia jinsi tunavyoweza kuvumilia
mfadhaiko wa kifikra au stress yote hayo yana nafasi muhimu katika uzima
wetu kimwili na kiakili. Suala jingine tunaloweza kulitaja hapa ni
matumizi ya vituo vya afya na hospitali. Jamii ambayo ina vituo vya afya
vya kutosha, vilivyo vizuri na vyenye kukidhi mahitaji ya watu wa jamii
hiyo, watu wake wana nafasi zaidi ya kuwa na siha nzuri kuliko jamii au
watu wanaoishi maeneo ambayo hayana vituo vya afya au hospitali. Kwa
mfano nchi zilizoendelea zenye vituo vya afya na hospitali za kutosha na
nzuri, watu wa nchi hizo huishi maisha marefu zaidi ikilinganishwa na
nchi masikini zenye upungufu katika sekta hiyo. Jinsia ya mtu pia
huathiri afya yake. Kuna magonjwa yanayowapata wanawake zaidi na kuna
magonjwa yanayowapata wanaume zaidi. Hali ya miili ya wanawake
hutofautiana na wanaume na hata kazi na shughuli wanazozifanya pia
huweza kuathiri afya zao kwa ujumla. Kwa mfano, kubeba mimba na
kujifungua, kansa ya ovari na kizazi huathiri afya ya wanawake katika
hali ambayo wanaume hupatwa na kansa ya tezi kibofu na ya korodani.
Wakati wa vita wanaume hushiriki kwa wingi kuliko wanawake na matokeo
yake ni kuuawa au kujeruhiwa. Wanawake na wasichana huenda wakawa
wahanga wa vitendo vya utumiaji mabavu dhidi yao na ukatili kuliko
watoto wa kiume na wanaume. Katika baadhi ya jamii watoto wa kike na
wanawake huwa hawapewi fursa ya kupata elimu na kujiendeleza kama
wanaume, suala ambalo huathiri afya zao pia. Tafiti nyingi zimeonyesha
ubaguzi wa kijinsia katika utoaji huduma za afya hata katika nchi
zilizoendelea.
Miongoni mwa mambo muhimu yanayoijenga afya ya
mwanadamu ni kula lishe salama na mlo uliokamilika. Tunaposema lishe
salama na mlo uliokamilika au healthy balanced diet kwa kimombo,
tunamaanisha masuala muhimu mawili. Moja ni kula kiwango kinachotakiwa
cha chakula kwa mujibu wa harakati na hitajio la mwili wako, na pili ni
kula aina tofauti za vyakula vinavyotakiwa ili kuijenga siha ya mwili.
Tunapaswa kufahamu kwamba, kula lishe bora ni suala muhimu linalochangia
kuimarisha afya ya mwili. Lishe salama na iliyokami inamaanisha kula
vyakula tofauti kutoka katika mafungu manne makuu ya vyakula na
kupunguza baadhi ya vyakula katika milo tunayokula kila siku.
Aina ya vyakula vinavyopaswa kuwepo
kwenye milo yetu ni pamoja na matunda na mboga kwa wingi. Kiwango cha
kutosha cha wanga kama vile mkate, wali, viazi, pasta na vinginevyo na
ni bora viwe vinatokana na aina mbalimbali za nafaka kamili
zisiokobolewa. Maziwa na vyakula vinavyotokana na maziwa kama mtindi na
jibini. Vyakula vyenye protini kama vyama, samaki, mayai, maharagwe na
vinginevyo na vilevile kiasi kidogo cha sukari , mafuta na chumvi.
ufuatao ni ushauri
au vidokezo muhimu (tips) kuhusiana na namna ya kula vyema ili
kuzilinda na kuziimarisha afya zetu. Tunashauriwa mlo tunaokula uwe na
kiasi cha kutosha cha wanga, kwani aina hiyo ya chakula huipa miili yetu
nguvu. Tunashauriwa kula matunda na mboga kwa wingi kila siku. Baadhi
wanasema, ni bora kula aina 5 za matunda tofauti na mboga kwa siku. Pia
tunashauriwa kula samaki kwa wingi kwa uchache mara mbili kila wiki na
kama hatutoweza kufanya hivyo au kwa wale ambao samaki wanawadhuru na
wale wasiokula nyama, wanapaswa kula virutubishi muhimu vinavyotupatia
mada zinazopatikana kwenye samaki kwa ajili ya afya ya miili yetu.
Tunashauriwa kupunguza kwa kiasi kikubwa sukari na mafuta katika milo
yetu. Vilevile tunashauriwa kula chumvi kwa kiwango kidogo, isizidi
gramu 6 kwa siku kwa watu wazima. Tunapaswa kufahamu kuwa, baadhi ya
vyakula tayari vina kiwango cha chumvi ndani yake kwani karibu theluthi
moja ya chumvi katika milo yetu hutoka katika vyakula ambavyo tayari
vimeshatengeneza kama supu iliyo tayari, sosi, mikate, asusa (snacks),
pai, pizza vyakula vinavyosindikwa na kuhifadhiwa. Hivyo kuna umuhimu wa
kula vyakula hivyo kwa kiasi kidogo. Hii ni kwa sababu ongezeko la
chumvi mwilini huweza kumfanya mtu apatwe na shinikizo la damu, hali
ambayo huweza kusababisha ugonjwa wa moyo na kiharusi. Suala jingine
tunalopaswa kuzingatia ni kunywa maji ya kutosha, tunashauriwa kila siku
kunywa kiasi cha gilasi 6 hadi 8 za maji au vyakula vingine vya
majimaji kama juisi na kadhalika, ili kuzuia upungufu wa maji mwilini.
Maji yana faida nyingi na baadhi yake ni kuusaidia mwili kuondoa kwa
urahisi sumu na mabaki yasiyotakiwa mwilini. Kusaidia kulainisha macho
na maungio ya mwili na pia hutusaidia wakati wa kumeza.
Jambo jingine tunaloshauriwa ni kuupa
mwili harakati, mazoezi ya mara kwa mara na kuwa na uzito unaotakiwa
kiafya. Jengine ni kutoacha kula kifuangua kinywa. Tunatakiwa kustaftahi
kila siku kwa sababu chakula hicho cha asubuhi huupa mwili nguvu ya
kuanzia siku na huamsha utendaji kazi wa mwili kwa ajili ya siku nzima.
Natumaini mmefaidika na kwa kuwa
kuvunjika kwa koleo sio mwisho wa uhunzi basi panapo majaaliwa.
kwa hisani ya Iran Swahili Radio
kwa hisani ya Iran Swahili Radio
0 comments:
Post a Comment