WATU FULANI HUDHANI kwamba kulala usingizi ni kupoteza
wakati. Wao huwa na shughuli nyingi za kibiashara na kirafiki kila siku,
na hulala tu wanapokuwa wachovu sana. Kwa upande mwingine, wengine
hutamani sana kupata usingizi mtamu lakini hujigeuza-geuza kitandani
hadi asubuhi.
Kwa nini baadhi ya watu hushindwa kulala, hali wengine wanatamani
sana kuwa macho? Je, tuuone usingizi kuwa starehe tu au ni muhimu? Ili
kujibu maswali hayo, ni lazima tufahamu mambo yanayotukia tunapolala.
Mambo Yasiyojulikana Kuhusu Usingizi
Kile kinachomfanya mtu apoteze fahamu na kulala usingizi bado
hakijulikani. Hata hivyo, watafiti wamegundua kwamba usingizi ni
utaratibu tata unaorudiwa na ubongo baada ya kila saa 24.
Tuendeleapo kuzeeka, mazoea yetu ya kulala hubadilika. Mtoto mchanga
hulala kwa vipindi vingi vifupi vyenye jumla ya saa 18 hivi kwa siku.
Kulingana na wataalamu wa usingizi, watu fulani wazima wanahitaji kulala
kwa muda wa saa tatu tu huku wengine wakihitaji muda wa saa kumi.
Uchunguzi wa hivi karibuni unaonyesha pia kwamba vijana fulani huona
ugumu wa kuamka asubuhi kwa sababu ya mabadiliko ya utendaji wa mwili.
Yaonekana mwili wa vijana hubadilika wanapobalehe, na ndiyo sababu wao
hutaka kulala usiku sana na kuamka wakiwa wamechelewa. Mazoea hayo ni ya
kawaida nayo huendelea hadi miaka ya katikati na ya mwisho ya ujanani.
Utendaji wa miili yetu huongozwa na kemikali zilizo mwilini na tayari
nyingi zinajulikana. Mojawapo ya kemikali zinazodhaniwa zinasababisha
usingizi ni homoni inayoitwa melatonin.
Homoni hiyo hutengenezwa kwenye ubongo,
na baadhi ya wanasayansi wanaamini kwamba ndiyo inayopunguza utendaji wa
mwili kabla tu ya usingizi. Homoni hiyo inapotengenezwa, joto la mwili
na damu inayoenda kwenye ubongo hupungua, na pole kwa pole misuli yetu
hulegea. Ni nini kinachotukia mtu anapoanza kulala usingizi?
“Njia Kuu ya Asili Inayoburudisha”
Muda wa saa mbili hivi baada ya kulala usingizi, macho yetu huanza
kusogea-sogea haraka. Jambo hilo limewafanya wanasayansi wagawanye
usingizi katika vipindi viwili: kipindi cha kusogeza macho haraka na
kipindi cha kutosogeza macho.
Kipindi cha kutosogeza macho kinaweza
kugawanywa katika vipindi vingine vinne vya usingizi mzito zaidi.
Vipindi hivyo viwili hubadilishana mtu anapolala usingizi mzito.
Mara nyingi, mtu huota ndoto wakati wa kipindi cha kusogeza macho. Pia
misuli ya mwili hulegea kabisa, na hivyo mtu huamka akiwa mchangamfu.
Isitoshe, watafiti fulani wanaamini kwamba habari mpya huhifadhiwa
katika kumbukumbu letu la kudumu katika kipindi hicho cha usingizi.
Wakati wa usingizi mzito (kipindi cha 3 na cha 4 cha kutosogeza macho),
shinikizo letu la damu na mpigo wa moyo hupungua zaidi, na hivyo
kupumzisha mzunguko wa damu na kumwepusha mtu na ugonjwa wa moyo. Zaidi
ya hilo, homoni nyingi za ukuzi hutengenezwa wakati wa kipindi cha
kutosogeza macho huku miili ya vijana fulani ikitengeneza homoni za
ukuzi mara 50 zaidi wakati wa usiku kuliko mchana.
Inaonekana usingizi huathiri pia hamu yetu ya kula. Wanasayansi
wamegundua kwamba kwa kweli usingizi ni “njia kuu ya asili
inayoburudisha” kama alivyosema Shakespeare.
Ubongo wetu huona ukosefu wa usingizi
kuwa ukosefu wa chakula. Tunapolala, mwili wetu hutengeneza homoni
inayoitwa leptin, inayojulisha mwili wetu kwamba tumeshiba.
Tunapokuwa macho kwa muda mrefu sana,
mwili wetu hutengeneza kiasi kidogo cha leptin, na kutufanya tutamani
sana chakula cha wanga. Kwa hiyo, kukosa usingizi kunaweza kutufanya
tule chakula kingi cha wanga, na hivyo tunenepe kupita kiasi.
Muhimu kwa Afya
Isitoshe, usingizi huwezesha mwili wetu kuharibu kemikali ambazo
inasemekana zinasababisha kansa na kufanya chembe zizeeke. Katika
uchunguzi wa hivi karibuni uliofanywa na Chuo Kikuu cha Chicago,
wavulana 11 wenye afya waliruhusiwa kulala kwa muda wa saa nne tu kwa
siku sita.
Baada ya kipindi hicho, chembe zao
zilifanya kazi kama chembe za watu wenye umri wa miaka 60, na kiwango
cha insulini kwenye damu yao kilikuwa kama kile cha mtu mwenye ugonjwa
wa sukari! Kukosa usingizi huathiri pia utengenezaji wa chembe nyeupe za
damu na homoni iitwayo cortisol, jambo ambalo humfanya mtu apate
maambukizo na magonjwa ya damu kwa urahisi.
Bila shaka,
usingizi ni muhimu kwa afya ya mwili na ya akili. Kulingana na mtafiti
William Dement, mwanzilishi wa kituo cha kwanza cha kuchunguza usingizi
katika Chuo Kikuu cha Stanford Marekani, “inaonekana kiwango cha
usingizi ambacho mtu hulala ndilo jambo muhimu zaidi ambalo huamua muda
atakaoishi.”
Deborah Suchecki, mtafiti kwenye kituo
cha kuchunguza usingizi huko São Paulo, Brazili, anasema hivi: “Kama
watu wangalijua jinsi kutolala usingizi kunavyoathiri mwili,
hawangalisema kwamba kulala ni kupoteza wakati au ni uvivu.”.
Lakini je, usingizi hupumzisha mwili nyakati zote? Kwa nini watu
wengine hulala usiku kucha na bado huamka wakiwa wachovu? Makala
inayofuata itakusaidia kutambua baadhi ya matatizo makubwa yanayoletwa
na ukosefu wa usingizi na itaeleza jinsi unavyoweza kupata usingizi wa
kutosha.
MATOKEO YA KUKOSA USINGIZI
MATOKEO YA MUDA MFUPI
▪ Kusinzia
▪ Hisia zinazobadilika- badilika
▪ Kusahau mambo kwa muda mfupi
▪ Kushindwa kupanga mambo na kuyatimiza
▪ Kutokuwa makini
MATOKEO YA MUDA MREFU
▪ Kunenepa kupita kiasi
▪ Kuzeeka mapema
▪ Uchovu
▪ Hatari kubwa ya kupatwa na maambukizo, ugonjwa wa sukari, magonjwa ya moyo, na matatizo ya tumbo
▪ Kusahau mambo sana
KULALA KIDOGO MCHANA
Je, umewahi kulemewa na usingizi baada ya chakula cha mchana? Hiyo
haimaanishi kwamba hukulala vyakutosha. Ni kawaida kusinzia wakati wa
mchana kwa sababu joto la mwili hupungua wakati huo.
Kwa kuongezea, hivi majuzi wanasayansi
wamegundua kwamba kuna protini inayoitwa hypocretin, au
orexin,inayotengenezwa na ubongo ambayo hutusaidia kuwa macho. Kuna
uhusiano gani kati ya hypocretin na chakula?
Tunapokula, mwili hutengeneza homoni inayoitwa leptin ambayo hutufanya
tuhisi tumeshiba. Lakini homoni hiyo huzuia utengenezaji wa hypocretin.
Yaani, kadirileptin inavyokuwa nyingi
kwenye ubongo, ndivyo hypocretin inavyopungua na tunahisi usingizi
zaidi. Labda hiyo ndiyo sababu katika nchi fulani watu hulala kidogo
baada ya kula chakula cha mchana.
kwa hisani ya manyanda healthy
Monday, 13 October 2014
- Blogger Comments
- Facebook Comments
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment